TUNDUMA:MUME WA ALIEJITOLEA KUKUMBATIA WATOTO AIBUKA MKOANI SONGWE ATOA KAULI

 Dar es Salaam. Mume wa Mariam Mwakabungu (25) aliyekuwa akijitolea kukumbatia watoto njiti waliotupwa na kutelekezwa katika Hosptali ya Rufaa ya mkoa Amana, Christopher Nyoni (29) amesema yupo tayari kumuunga mkono mkewe katika ajira yake mpya na kujiendeleza kielimu afikie ndoto zake.



Amesema mafanikio ya mkewe yametokana na hali ya wanandoa hao kusikilizana na kuamini upendo ni kwa watu wote.


Christopher ameyasema hayo leo Julai 21, 2023 wakati alipozungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu akiwa  Tunduma mkoani Songwe alikokwenda kwa shughuli zake za kibiashara.



"Niko tayari kumuunga mkono mke wangu katika suala la yeye kujiendeleza kielimu, nilimuunga mkono tangu mwanzo na nimefurahia sana kwasababu hatukutegemea kama tutasaidiwa hivi kwa uchumi wa sasa hivi tumefurahi sana nitamsapoti kujiendeleza kielimu kufikia malengo yake," amesema.


Christopher ambaye ni mfanyabiashara wa nguo za kiume, amewaasa wanaume kuwasilikiliza wake zao.


"Ninachowambia wanaume wanapaswa kuwa na moyo kwa sababu huwezi kujua, kuwasaidia watu ni kazi sana kwa sababu kuna mambo mengine ya kufanya unahitaji kuwa na imani na tumeumbwa kusaidia watu wengine, mwanamke anapokuja kutoa shida zake inabidi asilikilizwe," amesema.


Alipoulizwa kuhusu mapokeo yake mke alipomuomba kwa mara ya kwanza kwenda kusaidia mtoto njiti amesema;


"Sikuona ajabu kwa sababu mke wangu anapenda sana watoto kwahiyo alivyoniambia vile na namna watoto wenyewe walivyo, 'mume wangu naomba ruhusa nikawasaidie' nikamwambia sawa nikampa ruhusa aende."


Christopher amesema kwa upande wake alikuwa akiona ni jambo la kawaida licha ya kwamba aliachiwa majukumu ya familia.


"Nilikuwa naona ni kawaida kwa sababu nilikuwa nawaandaa watoto wanaenda shule na wakitoka huko kwa sababu nina dada yangu, nilikuwa nawachukua nawapeleka kule huku na mimi naendelea na majukumu mengine kwa sababu mke wangu alikuwa anakaa wiki moja au mbili akiwa Amana," amesema.


Christopher amesema licha ya majukumu hayo yote, haikumkatisha tamaa licha ya jamii kutoelewa sababu ya mkewe kutokuwepo nyumbani.


"Jamii ilikuwa inaona kawaida tu kwasababu sisi wenyewe hatukutegemea, iwapo kitazungumzwa kitu chohote kuhusu kujitolea kwake na tulifanya tu kama sehemu ya maisha na jamii ilikuwa inaniona mimi nawatengeneza tu watoto vizuri ninawapeleka shuleni wakawa wanajiuliza mbona mke hayupo ila hawawezi kuniambia.


"Mke alikosekana nyumbani ila tuliona ni kawaida tu alikuwa anaenda kuhudumia watoto ambao hatujui watakuja kuwa nani hapo baadae," amesema Christopher.


Amesema suala la ndugu zake walilichukulia kawaida kwa maana ni familia ambayo imekuwa ikitoa huduma kwa jamii ikiwemo huduma za kiafya.


"Ndugu zangu walisema, safi kama amejitolea kwenda kusaidia ni sawa na dada zangu wote hakukuwa na yeyote mwenye shida,"


Licha ya kumuamini na kumpa nafasi mkewe atoe upendo kwa watoto wasio wao, Christopher mwenye watoto wawili na Mariam wenye umri wa miaka 11 na saba amesema amejiajiri na amekuwa akijishughulisha na biashara.


"Shughuli zangu ni biashara za kawaida tu nasafiri mara nyingi naenda sehemu nyingi kama Tunduma, Nachingwea, Mbeya, Songea na Lindi," amesema Christopher.

Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE