DC MAHAWE AWAITA WANAMBOZI KUJIFUNZA NANENANE MBEYA

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Esther Mahawe ametoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo na Mkoa wa Songwe kwa ujumla kushiriki katika maonyesho ya kilimo, ufugaji na uvuvi maarufu Nanenane ili waweze kujifunza mambo mbalimbali.


Amesema kuwa maonyesho hayo yana lengo la kuwapa elimu wananchi katika sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi hivyo watumie fursa hiyo kutokana na wilaya hiyo kujihusisha na kilimo kwa asilimia kubwa na hakuna kiingilio.

"Niwasihi wananchi wa Mbozi na Mkoa wa Songwe kwa ujumla wafike kwenye maonyesho haya ili waweze kujifunza. Kuna mambo mengi ambayo wakifika watonufaika, maonyesho ya mwaka huu yamekuwa tofauti hivyo wakija hawataondoka bure" amesema 

 

Akiwa kwenye banda la maonyesho la Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi leo Ijumaa Agosti 4, 2023 Mkuu huyo wa Wilaya ya Mbozi ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk Francis Michael katika maadhimisho hayo amebainisha kuwa wananchi watapata firsa ya kuona mbegu bora za mazao na mifugo, kujifunza mbinu za kilimo na ufugaji bora pamoja na fursa ya kupata elimu ya mikopo ya kilimo kutoka katika taasisi za fedha.

Hata hivyo, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kwa maandalizi mazuri katika banda la halmashauri hiyo ambapo kuna vitu mbalimbali ikiwemo mbegu za mazao, kuku   pamoja na bidhaa mbalimbali za mazao zinazotoka katika wilaya hiyo.


Aidha, DC huyo ametoa rai kwa wakulima kujiunga kwenye vyama vya ushirika AMCOS huku akiwatoa hofu baadhi ambao wanawasiwasi kudhulumiwa katika vyama hivyo.


"Jana Waziri Mkuu alitoa maelekezo kwa Mkoa wa Songwe kusimamia AMCOS ili kuokoa kazi za wakulima. Niseme tu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa tayari tulishaanza kufanyia kazi maelekezo ya awali na tayati tumeshafanikiwa kusaidia Sh169 milioni kati ya Sh299 milioni zilizokiwa zimepotea kwenye mikono ya viongozi wa AMCOS 23 zimeokolewa na kazi bado inaendelea" ameeleza



Amesema kuwa bado wanaendelea kufanyia kazi maelekezo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ili kuhakikisha fedha za wakulima kwenye AMCOS hazitumiki vibaya.


DC Mahawe amemshukuru na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi hasa katika sekta ya kilimo.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

KUMBUKUMBU YA MAISHA YA MH. ESTER ALEXANDER MAHAWE

CONSTRUCTION OF THE ISONGOLE-ISOKO ASPHALT ROAD IS NOW OFFICIAL, CONTRACTOR INTRODUCED TO THE PUBLIC

*KUNDO AGOMA KUWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA MAJI VWAWA-MLOWO