DC MAHAWE AWAITA WANANCHI MBOZI KUUPOKEA MWENGE WA UHURU
Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Esther Mahawe amewataka wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru ambao unatarajiwa kupokewa Septemba 4 mwaka huu katika Kijiji cha Nanyala.
Mbio za Mwenge huo wa Uhuru zinatarajiwa kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inatekelezwa na Serikali ili kuwaboreshea na kuwasogezea karibu huduma wananchi.
DC Mahawe ametoa wito huo Agosti 23, 2024 akiwa katika mikutano wa hadhara kata za Nanyala na Ruanda ambapo akisema Mwenge wa Uhuru utapokewa kiwilaya katika Kijiji cha Nanyala kabla ya kuzungushwa kukagua na kuzindua miradi mbalimbali katika wilaya hiyo.
“Mwenge wa Uhuru unaleta upendo, umoja na mshimkamano na unaondoa chuki baina yetu kwa hiyo tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa ajili hiyo. Kazi hii imefanywa vizuri na viongozi wetu wa zamani akina Mwalimu Nyerere na wengine wengi. Ninazidi kutoa hamasa ya ninyi wananchi kualikana kwa wingi ili kuhakikisha kwamba hiyo mikesha yetu ya Mwenge inaenda vizuri tupokee mwenge hapa ili tuweze kuukimbiza kwenye maeneo mengine” amesisitiza mkuu huyo wa Wilaya.
“Utapita kwenye katika kata zisizozidi tano ila hizo zitawakilisha kata zawilaya yetu. Mwenge huo utazindua miradi zaidi ya Sh8 bilioni katika kata hizo. Kutakuwa na mradi wa maji, zahanati, maradi wa barabara ya lami, mradi wa tofali unaotokana na mapato ya ndani ya halmashauri na mradi wa excavator” amesema Mkuu huyo wa wilaya akibainisha baadhi ya miradi ambayo itazinduliwa na Mwenge wa Uhuru.
Amesema kuwa miradi hiyo imesimamiwa vizuri na halmashauri hivyo ikizinduliwa itakuwa inasaidia kuongeza mapato ya halmashauri na kurahisisha huduma kwa wananchi.
Amesema kuwa miradi hiyo itakayopitiwa na Mwenge ni baadhi tu ya miradi lakini Serikali inatekeleza miradi mingi katika Wilaya hiyo ambapo Mwenge huo hautaweza kukimbizwa katika miradi yote.
Comments