TAKUKURU SONGWE YATOA TAARIFA YAKE YA MIEZI MITATU



Taasisi ya Kuzuai na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Songwe imewataka wananchi katika mkoa huo kutoa ushirikiano wa taarifa za rushwa kwa kuwa ipo sheria ya kuwalinda watoa taarifa hizo.


Pia, imesema kuwa zipo sheria ambazo zinawabana maofisa wa taasisi hiyo kutoweka wazi wanaowapa taarifa za rushwa hivyo wananchi wasiogope kutoa taarifa pale wanapobaini kuwa kuna viashiria vya rushwa hasa kwenye miradi ya maendeleo.


Hayo yamesemwa leo Alhamisi Agosti 3, 2023 na Mkuu Takukuru Mkoa wa Songwe, Edings Mwakambonja wakati akitoa taarifa ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni mwaka huu kwa waandishi wa habari.


Amesema kuwa Takukuru Rafiki imesaidia kuiweka taasisi hiyo karibu na wananchi kutokana na elimu wanayoitoa ambayo imesaidia wananchi kuondoa hofu.


“Katika kipindi cha Aprili mpaka Juni tumefanikiwa kufika katika kata 15 kutoa elimu na kusikiliza kero za wananchi. Kero 84 zilitolewa na kati ya hizo kero 41 zilishatatuliwa na zilizobaki zinaendelea kushughulikiwa” amesema 

“Kwa sasa wananchi wanaelewa na wanatoa ushirikiano hasa katika kata tulizoenda kutoa elimu na kusikiliza kero zao. Kuhusu kuwalinda wanaotoa taarifa za rushwa kuna sharia za kuwalinda hivyo wananchi wasiogope watupe taarifa” amesisitiza 

Mwakambonja amesema taasisi hiyo ipo kwenye utekelezaji wa kutoa elimu kupitia Takukuru Rafiki katika kata zote 94 za mkoa wa Songwe ambapo mpango huo ni endelevu.

Akizungumzia juu ya uchunguzi na mashtaka katika kipindi hicho cha miezi mitatu, Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Songwe amesema kuwa kati ya kesi mpya 14 zilizofunguliwa mahakamani kesi nne zimeamuliwa na kesi zote nne washtakiwa walitiwa hatiani.


Amesema kuwa taasisi hiyo ilipokea malalamiko 33 ambapo 23 yalikuwa yanahusu rushwa huku 10 yakiwa hayahusu rushwa katika kipindi cha miezi mitatu.


“Kesi mpya 14 zilifunguliwa mahakamani ambapo kesi 10 zinaendelea na kesi nne ziliamuliwa. Kesi zote nne washtakiwa walitiwa hatiani na kurejesha fedha” amebainisha

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

UDUMAVU BADO TISHIO -DUGANGE

SONGWE JOGGING WARUDI NA MEDANI ZAIDI YA KUMI NA TANO TULIA MARATHON

MOMBA HAWANA JAMBO DOGO: ROUTE VIONGOZI NA WANANCHI WAKUTANA PAMOJA ROUTER MATCH YANOGA