NAIBU WAZIRI WA UJENZI AFANYA ZIARA KUKAGUA MIUNDOMBINU YA BARABARA WILAYANI SONGWE
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amefanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara katika Wilaya ya Songwe.
Waziri huyo amefanya ziara hiyo leo Jumatano Oktoba 4, 2023 ambapo ametembelea na kukagua daraja la Gulula, eneo la Zira ambalo linatarajiwa kuanza ujenzi wa tuta la kuzuia maji wakati wa mvua pamoja na kipande cha barabara ya lami cha Mkwajuni-Saza chenye urefu wa mita 400 kilichojengwa kwa thamani ya zaidi ya Sh300 milioni.
Katika ziara hiyo, Mhandisi Kasekenya ameiagiza TANROADS Mkoa wa Songwe kuharakisha ujenzi wa tuta hilo katika eneo la Zira kabla msimu wa mvua haujaanza huku akiwataka wananchi kutunza miundombinu ya barabara.
Waziri huyo ambaye aliambatana na wataalamu wake akiwemo Meneja wa Tanroads Mkoa wa Songwe, Suleiman Bishanga walipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Mhe. Solomon Itunda, Katibu Tawala wa Wilaya ya Songwe, Reuben Chongolo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe, Abdallah Mgonjwa wakuu wa taasisi mbalimbali za wilaya hiyo na wataalamu kutoka Halmashauri.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe. Itunda amemshukuru Naibu Waziri huyo kwa kufanya ziara huku akimuomba asukume utekelezaji wa ujenzi wa daraja la Galula kwa wakati ili kurahisisha usafiri hasa kipindi cha mvua.
Pia, Mhe. Itunda amemuomba Naibu Waziri huyo kusukuma mchakato wa ujenzi wa barabara ya Mbalizi-Mkwajuni-Sanza yenye urefu wa kilomita 86 kwa kiwango cha lami.
Mkuu huyo wa Wilaya amemshukuru Rais wa JMT, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwaajili ya miradi ya maendeleo katika Wilaya hiyo huku akiahidi kuwa wilaya hiyo itaendelea kuisimamia na kutoa elimu kwa wanananchi ili wazidi kutunza miundombinu inayojengwa katika maeneo yao.
Comments