MCHEZAJI MPYA SIMBA KUANZA NA KOMBE LA MAPINDUZI



 BAADA ya dili lake la usajili kukamilika kwa asilimia mia moja, kiungo mpya wa Simba, Ladack Chasambi anatarajiwa kukiongoza kikosi hicho katika Kombe la Mapinduzi katika msimu huu.

Chasambi ni kati ya wachezaji wapya waliokuwa wanawindwa vikali na baadhi ya klabu za hapa nchini kutokana na kiwango bora ambacho anakionyesha akiwa anaichezea Mtibwa Sugar ya Turiani, Manungu mkoani Morogoro.

Michuano hiyo inatarajiwa kuanza kufanyika Desemba 28, mwaka huu huko Unguja, Zanzibar.

Taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, ni kuwa kiungo huyo dili lake limekamilika kwa asilimia mia moja ndani ya Simba, kilichobakia kwake ni kutambulishwa pekee.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kiungo huyo mara baada ya kutambulishwa rasmi ataanza kuichezea timu hiyo katika Kombe la Mapinduzi

Aliongeza kuwa kiungo huyo anatarajwa kuwepo katika msafara wa timu hiyo, utakaosafiri kwenda Zanzibar ndani ya siku hizi mbili kujiandaa na michuano hiyo.

“Ladack usajili wake umekamilika kwa asilimia kubwa, na yeye huenda akawa mchezaji wa kwanza kutambulishwa katika timu.

“Pia kiungo huyo anatarajiwa kuanza kuichezea timu hiyo, katika Kombe la Mapinduzi ambalo wamethibitisha kushiriki katika msimu huu.

“Kiungo huyo amesajiliwa baada ya kufikia makubaliano mazuri na Mtibwa Sugar ambayo tumemnunua kwa mkataba wa miaka mitatu,” alisema mtoa taarifa huyo.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema kuwa: “Tumepanga kukifanyia maboresho makubwa kikosi chetu kupitia usajili huu wa dirisha hili kubwa ambao umefunguliwa hivi karibuni.”

Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE