MTUHUMIWA MMOJA ASHIKILIWA NA DAWA ZA KULEVYA, ULINZI WAIMARISHWA MKOANI MBEYA KUELEKEA MWAKA MPYA 2024.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Kelvin Amanyisye [19] Mkazi wa Lubele- boda ya Kasumulu kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya aina ya Bhangi kilogramu 13.
Akizungumza na waandishi wa habari Desemba 30, 2023 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi wa Polisi Benjamin E.Kuzaga amesema kuwa Mtuhumiwa alikamatwa Desemba 28, 2023 katika kivuko kisicho rasmi kiitwacho boda ya zamani kilichopo Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya akiwa na bhangi hiyo ikiwa kwenye mifuko ya rambo 13 na kufichwa kwenye begi kubwa na kuisafirisha kwa kutumia Pikipiki MC 366 aina ya Boxer.
Mtuhumiwa alikuwa akielekea Stendi ya Mabasi Kyela kwaajili ya kusafirisha dawa hizo za kulevya kuelekea Dar es Salaam. Atafikishwa Mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kuelekea sikukuu ya mwaka mpya 2024 limejipanga vizuri kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa mtu/watu ambao hawana kibali cha kupiga/kufyatua fataki kutopiga kwani hadi tarehe ya leo ni mtu mmoja pekee aliyeomba Kibali cha kupiga fataki na kukubaliwa.
Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa katazo la kuchoma moto matairi katika barabara kwani husababisha uharibifu na usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara hizo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kufanya hivyo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu. Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawatakia wananchi wote wa Mkoa wa Mbeya na Tanzania kwa Ujumla Kheri ya Mwaka Mpya 2024 huku likiwakumbusha kusherehekea kwa amani na utulivu.
Comments