WATELEKEZA LORI NA PIKIPIKI SITA ZILIZOBEBA BANGI
POLISI mkoani Morogoro inamsaka dereva wa lori aina ya Mitsubishi Fuso lenye namba za usajili T.301 DPQ lenye tela namba T. 562 DNV mali ya Kampuni ya K.T. Abri alilolitelekeza.
Ndani yake imekutwa mifuko 30 ya dawa za kulevya aina ya bangi ikiwa na uzito wa kilo 430 kando ya Barabara Kuu ya Morogoro- Iringa katika Kata ya Mangae , Wilaya ya Mvomero.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Alex Mkama amesema hayo Desemba 31, 2023, na kusema Polisi walikuwa wanafuatilia nyendo za gari hilo baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu usafirishaji dawa za kulevya aina ya bangi kwenda Dar es Salaam.
“Tuliweka mtego eneo la Kijiji cha Soli, Kata ya Mangae. Katika mtego huo tumefanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya bangi mifuko 30 yenye kilo 430 na pikipiki sita ambazo zilikuwa zinatumika kusafirisha kutoka mbali inakolimwa na kuletwa maeneo haya ya barabarani …lakini kwa bahati mbaya waliweza kukimbia kabla ya kukamatwa kwao, “ amesema Mkama.
Mkama, amesema wameamua kushikilia Pikipiki hizo sita ili kuwapata wamiliki wake ka lengo la kuwapata madereva wake pamoja na mmiliki wa Lori hilo ili kufanya naye mahojiano kuhusu hizo dawa zilizizokamatwa.
Kamanda Mkama amesema kuwa Lori hilo ndani yake lilibeba chakula cha kuku mifuko 359 kikisafirishwa kutoka mkoani Iringa kwenda jijini Dar es Salaam.
“Njia aliyoitumia kati kati ya mifuko ya chakula cha kuku ameiweka mifuko ya bhangi na kwenye ukaguzi wa kawaida si rahisi kwa Polisi kuweza kubaini au kung’amua lazima uwe na taarifa sahihi.” Amesema Mkama.
Comments