CCM SONGWE YAIPONGEZA RUWASA KWA UTEKELEZAJI WA MIRADI.


Katika kutekeleza kwa vitendo dhana ya kumtua mama ndoo kichwani, Wakala wa Maji Vijijini Wilaya ya Momba Mkoani Songwe unajenga mradi wa Maji wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Billion moja katika vijiji vya Isanga na Kakozi na unatarajiwa kukamilika kufikia Juni 24, 2024.


Hayo yamethibitika kwenye ziara ya Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Songwe ambayo inaendelea kuifanya Mkoani humo baada ya kutembelea na kukagua mradi wa Maji Kakozi Isanga ambapo Tank kubwa linajengwa katika kijiji cha Kakozi na Kisima kirefu kilishachimbwa katika kijiji cha Isanga.

Akizungumza kwenye ziara hiyo ya ukaguzi wa miradi, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Songwe Radwell Mwampashi, amempongeza Meneja wa usambazaji Maji Vijijini RUWASA Mkoa wa Songwe Charles Pambe na yule wa Wilaya ya Momba Beatus Katabazi, kwa utekelezaji na usimamizi mzuri wa miradi ya Maji Mkoani humo.


Amewataka wakuu wa idara nyingine kuiga mfano kwa RUWASA ambao anasema wanafanya kazi nzuri na kukiuza zaidi Chama Cha Mapinduzi kwa wananchi ambao ndio walipa kodi.


"Kwakweli mimi huwa sina unafiki nikisema kitu nasema kutoka moyoni, nakupongeza sana Meneja wa RUWASA Mkoa wa Songwe na Meneja wa Wilaya hii ya Momba mnafanya kazi nzuri na idara nyingine za Umma ziige kwenu (RUWASA)", Amesema Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Songwe Radwell Mwampashi.


Akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini RUWASA Wilaya ya Momba Beatus Katabazi, amesema mradi wa maji Isanga Kakozi wamedhamiria kujenga vituo nane vya kutochea maji kwa ajili ya vijiji hivyo viwili.


"Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Songwe na Kamati ya Siasa kuna ujenzi wa vituo nane vya kuchotea maji ambapo vituo vinne vitajengwa katika kijiji cha Kakozi na vinne katika kijiji cha Isanga. Matarajio yetu ni kumaliza mradi huu Juni 24, 2024 na tukipata tu fedha za mabomba tutaanza mara moja kazi ya kuchimba mitaro kwa ajili ya ulazaji wa bomba", amesema Katabazi.


Amesema utekelezaji huo wa mradi ulianza mwezi wa tisa mwaka 2023 hivyo baada ya kupokea mabomba wataanza kazi ya kuchimba mitaro ili kuharakishwa kujengwa kwa mradi huo kwa maslahi ya wananchi.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe (Kamisama wa CCM) Dkt. Francis Michael, amewapongeza RUWASA kwa utekelezaji wa miradi kwa weledi na kubainisha changamoto kubwa kuwa ni ucheleweshaji wa fedha hivyo kuhimiza uharakishwaji fedha kutoka Serikali kuu ili miradi itekelezwe kwa wakati jambo ambalo ameahidi kuendelea kulifuatilia kwa RUWASA makao makuu.


Naye Diwani wa Kata ya Ndalambo Mhe. Fravian Sichizya, amesema mradi wa Maji Isanga Kakozi utakuwa mkombozi kwani wananchi wake hasa katika Kijiji cha Kakozi walikuwa wakitumia muda mrefu kutafuta huduma ya maji safi na kuathirika kiafya badala ya kujikita kwenye uzalishaji mali.


Peter Simbeye ni mkazi wa Kijiji kijiji cha Kakozi Kata ya Ndalambo, ameishukuru Serikali kwa kuanza kujenga mradi huo anaosema utawasaidia hasa akina mama na adha ya maji ambayo kwa muda mrefu imekuwa kero.


Christina Simkonda mkazi wa Kijiji cha Isanga Wilaya ya Momba, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kuendelea kutekeleza miradi kwa vitendo.

Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE