CHIKOTI AWATANGAZIA KIAMA WAZAZI WASIOWAPELEKA SHULE WATOTO,MSAKO NYUMBA KWA NYUMBA KUANZA
KUTOKANA na idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kusuasua katika halmashauri ya wilaya ya Momba mkoani Songwe,uongozi wa wilaya hiyo umetangaza kuwachukulia hatua wazazi au walezi watakaokwamisha watoto kujiunga na shule walizopangiwa.,,anaripoti Ibrahim Yassin Songwe.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi,leo Januari 28/2024 mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo,Mathew Chikoti amesema bado hali ya watoto kuripoti shule haijawa nzuri hivyo walianza kutoa elimu kupitia mikutano na kila mzazi anajua wajibu wa mtoto kusoma.
Amesema baada ya kutoa elimu kwa wazazi hao,wataanza kutembea nyumba kwa nyumba mtaa kwa mtaa hadi mashambani kuwasaka watoto ambao hawajatipoti shule na kuwachukulia hatua kali za kisheria wazazi watakaoshindwa kuwapeleka watoto shule.
‘’Ndugu mwandishi suala la mtoto kwenda shule sio ombi ni lazima,mtoto licha ya kuzaliwa na baba na mama lakini ni wa Serikali hivyo anapaswa kupata haki yake ya kimsingi kwa kwenda shule,serikali imetumia fedha nyingi kujenga shule kazi ya mzazi ni kumpeleka shule mtoto na si vinginevyo’’amesema Chikoti.
Chikoti ambaye pia ni Diwani wa kata ya Mkulwe,alisema kama ni elimu wameisha itoa na serikali imeruhusu mwanafunzi aripoti shule hata akivaa nguo za nyumbani aendelee na masomo wakati wazazi wakitafuta fedha za kuwashonea sare na mahitaji mengine.
Siku za hivi karibuni katibu tawala mkoani Songwe,Happiness Seneda alifanya ziara wilayani humo kukagua ukamilishaji wa mradi wa ofisi ya mkuu wa wilaya,na kupitia kuoana umaliziaji wa ujenzi wa shule mpya ya Naming’ong’o ambapo alikuta wanafunzi 35 kati ya 78 wameripoti na kutoa maagizo.
Seneda licha ya kuridhiswa na ujenzi wa miradi hiyo,alimuagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo,Manoza Fabian na katibu tawala wa wilaya ya Momba,Frank Mkinda kushirikiana na viongozi wa vijiji kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa wanaripoti shule.
Akiyapokea maagizo hayo,mkurugenzi Fabian amesema watahakikisha watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanaripoti licha ya changamoto iliyopo kuwa Momba ni wilaya ya kilimo baadhi ya wazazi wanaenda na watoto mashambani badala ya kuwapeleka shule,watahakikisha wanachukua hatua.
Afisa mtendaji wa kata ya Chitete Luben Silvester amesema awali wanafunzi walikuwa wakitembea kilometa zaidi ya 20 kwenye shule mama ya Chitete,lakini serikali imesikia kilio cha wananchi imejenga shule mpya kuwasogezea shule kuwahepusha watoto kutembea umbali huo.
Amesema Chitete ni makao makuu ya wilaya,yenye idadi ya watu 29,133 ikiwa na kaya 6,608,ujenzi wa shule mpya Naming’ong’o upo asilimia 75,mwaka huu imeandikisha wanafunzi 78 wa kidato cha kwanza walioripoti ni 35,shule mama Chitete waliandikishwa 284 walioripoti 180 kazi ya kuwasaka wasioripoti inafanyika.
Comments