WANAFUNZI 8 WALIOKATALIWA WAFAURU GEITA

 WANAFUNZI wanane waliokataliwa na shule mbalimbali za taasisi binafsi mkoani Geita kutokana na ufaulu mbaya wamegeuka mashujaa baada ya kupata matokeo mazuri katika mtihani wa kidato cha nne 2023.

Wanafunzi hao walibahatika kupata nafasi ya usajili wa masomo na kituo cha mtihani katika shule za taasisi ya Royal Family ya mjini Geita mwaka 2022 ambapo wamehitimu na kufaulu vizuri.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Royal Family ya mjini Geita, Elikana Simon amewaambia waandishi wa habari mara baada ya Baraza la Mtihani la Taifa (NECTA) kutangaza matokeo ya kidato cha nne 2023.

Elikana amesema wanafunzi hao walikuwa wamekataliwa na shule tofauti kwa madai ya kuwa na ufaulu mbaya kwenye mitihani ya majaribio lakini shule hiyo ilijidhatiti kuwapokea kwani elimu ni huduma.

Amebainisha awali wanafunzi hao walikuwa tisa lakini mmoja hakuhitimu kwa changamoto za kiafya huku nane waliohitimu wanne wamepata daraja la kwanza, watatu daraja la pili na mmoja daraja la tatu.

“Kwa hakika watoto wetu wametuwakilisha vizuri sana, wamefanya kile ambacho tumekitarajia, wametimiza malengo yao, na malengo yetu kama walimu, na malengo ya jamii nzima na wazazi wao.”

Mkurugenzi wa Taasisi ya Royal Family, Mhandisi Lazaro Philipo ameeleza watoto hao wengine walikuwa wamekataliwa kwa changamoto za kinidhamu huko walikotoka lakini yeye alijidhatiti kuwabadilisha.

Amesema Kauli Mbiu ya shule yake ni kuwa kielelezo hivo japokuwa baadhi ya walimu hawakuwa tayari kuwapokea wanafunzi hao lakini yeye aliwekea mkazo na msisitizo wapokelewe na wasaidiwe.

“Maana halisi ya sisi kuwa kielelezo ni kumwambia mwanafunzi kwanza ajue kuwa yeye siyo mtu wa kawaida akitambua hiyo thamani iko ndani yake.” Amesema na kuongeza;

“Wengine walikuja wamekata tamaa hasa kwenye masomo ya sayansi na wazazi wao walikuwa wanatamani watoto wao wafanye vizuri kwenye masomo hayo lakini walikuwa wameshindwa kabisa.


“Sisi walipokuja cha kwanza tulichowaambia kwamba nyinyi mnaweza, kwa nini wengine wanaweza na nyinyi msiweze, kwa hiyo tukatumia muda wa kuwahamasisha wajione kwamba wanaweza.”

Mhandisi Lazaro amebainisha pia wanafunzi hao walipatiwa mlezi wa kitaaluma na shule ikawekeza katika mafunzo ya vitendo na kufanikiwa kuwabadili watoto hao kuwa mashujaa.

Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE