BITEKO AFUTA LIKIZO ZA WAFANYAKAZI TANESCO
Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko ametangaza kufuta likizo kwa watumishi wote wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) akiwataka wote wawe kazini kukabiliana na changamoto ya upungufu wa umeme.
Amesema hakuna mtumishi wa Tanesco atatakiwa kwenda likizo wakati huu wa changamoto ya mgawo wa umeme na kwamba, kila mmoja kwenye eneo lake atatakiwa kufanya kazi kwa bidii.
Dk Biteko, ambaye pia ni Waziri wa Nishati ametoa agizo hilo leo Ijumaa, Februari 23, 2024 wakati alipotembelea chanzo cha kuzalisha umeme cha Kidato mkoani Morogoro.
Naibu Waziri Mkuu huyo yupo kwenye ziara kukagua vyanzo vya kuzalisha umeme, kuangalia shughuli za uzalishaji ikiwa ni mkakati kumaliza changamoto ya upungufu wa umeme nchini.
Hatua hiyo ya Dk Biteko imetokana na kupewa taarifa kwamba, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Morogoro, kuwa amekwenda likizo.
“Huu ni muda wa kukimbiza kutatua changamoto zilizopo mbele yetu. Nitoe wito kwa uongozi wa Tanesco kuwa hakutakuwa na likizo kipindi hiki ambacho watanzania wanakabiliwa na changamoto ya umeme.
Hakuna likizo tena kuanzia sasa hivi kwenda mbele kwa mtu yeyote anayefanya kazi Tanesco. Nilivyosema Tanesco hamtalala wakati huu wa mgawo nilikuwa naaminisha, haiwezekani tuko kwenye changamoto halafu kuna wengine wanataka kulala.
Sisi wenyewe tunazunguka kila mahali kuhakikisha wananchi wanapata umeme. Katika hili tutachukua hatua kwa aliyeidhinisha likizo n ahata huyo aliyeomba likizo wakati huu ametoa wapi ujasiri,” amesema Dk Biteko.
Comments