KATAVI WAPOKEA TANI 30 ZA SUKARI
MPANDA, Katavi: MKUU wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuf amewataka wafanyabiashara mkoani Katavi kuzingatia bei elekezi ya sukari Sh 3200 kwa kilo moja na asiwepo wa kumuuzia mwananchi bei zaidi ya iliyoelekezwa.
Akizungumza wakati wa upokeaji wa tani 30 za sukari mkoani Katavi, mkuu huyo wa wilaya amekiri kulikuwa na changamoto kubwa ya sukari wilayani humo hivyo ujio wa tani hizo utapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto hiyo wakati sukari nyingine ikisubiriwa kuingia wilayani humo kuanzia wiki ijayo.
Kiongozi huyo pia amewataka wananchi kutoa taarifa endapo watauziwa bei tofauti na iliyo elekezwa na atakayebainika kuuza kinyume na bei hiyo atachukuliwa hatua za kisheria.
Naye, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Viwanda Biashara na Uwekezaji Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Katavi, Florence Chrisant amesema kuanzia wiki ijayo mkoa utapokea tani 214 ambazo zitaondoa kabisa tatizo la uhaba wa sukari kwa asilimia 100 mkoani humo.
Hata hivyo wananchi wa Mpanda wameishukuru Serikali kwa kuiona changamoto hiyo huku wakiomba kuongezewa zaidi sukari ili changamoto hiyo isijirudie.
Comments