SILINDE AWATAKA WATAFITI WA KILIMO KUONGEZA KASI YA UTAFITI
MOROGORO: WATAFITI wa kilimo nchini wametakiwa kuongeza kasi katika kufanya tafiti za kilimo kwa kuwa upo uhitaji wa upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima zenye kuendana na mabadiliko ya tabia nchi.
Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde ameiwaambia watafiti hao alipotembelea Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), Kituo cha Ilonga kilichopo Kilosa, Morogoro.
“Kuna hitaji la upatikanaji mbegu bora kwa wakulima zenye kuendana na mabadiliko ya tabia nchi na kuhimili magonjwa.
“Kutokana na hitaji hilo, watafiti mnapaswa kuongeza jitihada za kufanya tafiti na usambazaji teknolojia za kilimo ili kuongeza tija katika mnyororo mzima wa sekta ya kilimo,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Thomas Bwana amesema taasisi hiyo imejipanga kutafiti na kusambaza teknolojia za kilimo zenye kukidhi mahitaji.
Ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika kuandaa wataalamu wa kufanya tafiti zinazotatua changamoto mbalimbali za kilimo.
Pia amesema TARI ina miundombinu ya kisasa ambayo inaendelea kuboreshwa ikiwemo maabara na mashamba ya kufanyia tafiti katika maeneo mbalimbali.
Naye Mkurugenzi wa kituo cha TARI Ilonga Dk. Emmanuel Chilagane amewataka wakulima kuendelea kutumia teknolojia zinazogunduliwa na taasisi hiyo zenye kuendana na mabadiliko ya tabia nchi ili kuongeza kipato cha mtu mmoja na taifa kwa ujumla.
Comments