BILIONI 431.474 KUIFUNGUA KAGERA KIMIUNDOMBINU
Katika kipindi cha miaka mitatu, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe Rais Dkt. Samia Hassan imetoa zaidi ya shilingi bilioni 431.474 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya ujenzi wa Miundombinu ya barabara na madaraja Mkoani Kagera.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanroads Mkoa wa Kagera, Mha. Ntuli Mwaikokesya amesema hayo leo tarehe 20 Machi 2024 alipozungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya ujenzi.
Amesema fedha hizo zimeweza kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati iliyokamilika na inayoendelea kujengwa ambayo ni pamoja na Ujenzi wa barabara ya Nyakanazi –Kidahwe; kipande cha Nyakanazi- Kabingo (Km 50), barabara ya Bugene-Kasulo- Kumunazi (Km 128.5), kipande cha Bugene - Burigi chato (Km 60), Ujenzi wa daraja la kitengule (140m) na barabara unganishi (km 18) na Ukarabati wa barabara ya Lusahunga–Rusumo (km 92) kwa kiwango cha lami.
Miradi mingine ni Ujenzi wa barabara ya kutoka Kagera sugar Juntion(Bunazi) –Kagera Sugar –Kitengule Junction (Km 25), Ujenzi wa barabara ya Omurushaka (Chonyonyo) – Nkwenda - Kyerwa (Km 50) kwa kiwango cha lami, pamoja na Upanuzi wa njia nne wa barabara ya Bukoba (Rwamishenye round about) – Bukoba Port Km 5.1.
“Tunamshukuru Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, ndani ya Miaka hii mitatu, tumeweza kutekeleza zaidi ya miradi minne ya ujenzi ikiwemo Daraja la kitengule ambalo ni mkombozi mkubwa kwenye kiwanda cha sukari cha Kagera ambacho kimefungua fursa na kuongeza vipato vya Wananchi wanaotumia daraja hilo kwenda Kiwandani” ameeleza.
Amesema katika kipindi hicho zaidi ya taa za barabarani 486 zimewekwa katika wilaya ya Bukoba mjini, Karangwe, Kyerwa, Ngara, Biharamulo pamoja na Muleba, na katika mwaka wa fedha wa 2023/24 wanatarajia kuongeza taa takribani 573 ili kuweza kufunga Mkoa mzima wa Kagera.
Naye Mkandarasi Mzawa anayejenga na kufanya Upanuzi wa njia nne wa barabara ya Bukoba (Rwamishenye round about) – Bukoba Port Km 5.1, Mha. Martin Kamala, ameishukuru Serikali ya Awamu ya sita kwa kuwajali na kuwapa kipaumbele katika kutekeleza miradi mikubwa na midogo Nchini.
Comments