RAIS AJIUZULU AANDIKA BARUA
Rais wa Vietnam, Vo Van Thuong ametangaza kujiuzulu jana Machi 20, 2024 ikiwa ni baada ya kukaa mwaka mmoja madarakani. Bunge la nchi hiyo limeidhinisha kujiuzulu kwake.
Sababu ya kuchukua hatua hiyo imetajwa kuwa ni ukiukaji wa kanuni za chama, kulingana na ripoti za ndani nchini humo, pamoja na mapungufu aliyonayo rais huyo wakati ambao nchi hiyo ipo kwenye kampeni ya kupinga ufisadi.
Uamuzi wa Bunge umekuja baada ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti jana Jumatano kukubali uamuzi wa Rais huyo, aliyehudumu kuanzia Machi 2, 2023.
Imeelezwa ukiukwaji na dosari zake zimeathiri vibaya mtazamo wa umma pamoja na sifa ya chama na serikali, japokuwa haijafafanuliwa zaidi juu ya dosari hizo.
Thuong anakuwa Rais wa pili kujiuzulu katika kipindi cha miaka miwili huku kukiwa na operesheni kali dhidi ya ufisadi ambao umesababisha baadhi ya wanasiasa kufukuzwa kazi, na viongozi wakuu wa biashara kushitakiwa kwa udanganyifu na ufisadi.
Thuong, mwenye umri wa miaka 54, alikuwa Rais mwenye umri mdogo zaidi wa Vietnam alipochaguliwa kwa muhula wa 2021 hadi 2026 baada ya mtangulizi wake Nguyen Xuan Phuc kujiuzulu, huku muhula wake ukiwa mfupi zaidi katika ya hivi karibuni nchini humo.
Kufuatia kujiuzulu kwake Makamu wa Rais wa sasa Vo Thi Anh Xuan atakuwa Rais wa muda.
Comments