POLISI WAPYA 68 WAWASILI MKOANI SONGWE
Askari wapya kutoka shule ya Polisi Moshi wamepokelewa Mkoani Songwe tarehe 27, Machi 2024 baada ya kuhitimu mafunzo yao ya awali Machi 25 mwaka huu wakiwa wako tayari kwa ulinzi wa raia na mali zao Mkoani humo.
Askari hao wamepokelewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Agustino Senga na kuwataka kufanya kazi kwa uweledi ili kuendelea kulinda taswira nzuri ya Jeshi la Polisi kwa jamii.
"Tutakuwa nanyi kwa miezi miwili kwa lengo la kuendelea na mafunzo ya nadharia na vitendo ili kuwaongezea maarifa katika utendaji wa kazi zetu za kila siku ikiwa ni pamoja na kuyatambua maeneo yenu ya kazi mkiwa mnayafanya kwa vitendo yale yote mliyofundishwa ili kuendelea kuzuia uhalifu na wahalifu Mkoani hapa" alisema kamanda Senga.
“Askari mnatakiwa kutojihusisha na vitendo ambavyo vinaleta taswira mbaya kwa Jeshi la Polisi, mnapaswa kufanya kazi kwa kufuata wimbo wa maadili ya Afisa wa Jeshi la Polisi na kuzingatia kauli mbiu yetu ambayo nidhamu, haki, weledi na uadilifu” alisisitiza Kamanda Senga.
Jumla ya askari 68 wamepokelewa Mkoani Songwe ikiwa ni mafanikio ya miaka 03 ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ambapo ameendelea kutoa ajira kwa Jeshi la Polisi ili kuendelea kuzuia na kutanzua uhalifu na wahalifu katika Taifa letu.
Comments