RC DODOMA ATOA WITO KWA SHULE KUJENGA ENEO LA SHULE



 MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ametoa wito kwa shule zote zilizopo Mkoani Dodoma kuhakikisha zinatafuta maeneo kwaajili ya michezo kwa wanafunzi kwasababu michezo inajenga  afya ya akili na mwili.

Wito huo aliutoa katika hafla ya uzinduzi wa wiki ya wadau wa elimu kwa Mkoa wa Dodoma pamoja na ugawaji wa mipira 1000 kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kwa Halmashauri zote zilizopo Dodoma lengo likiwa kuwasaidia wanafunzi kuendelea kujifunza michezo kwa ufanisi.

“Nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono sekta ya michezo kwa kuhakikisha Tanzania inajiandaa kushindana katika mashindano makubwa duniani, pia kwa kuwaandaa vijana kwaajili ya kuitumikia timu ya Taifa na kufanya vizuri katika sekta ya michezo duniani. Nitoe shukrani kwa uongozi wa TFF kwa kutuwezesha mipira ambayo itatumika katika kuinua vipaji kwa wanafunzi katika mkoa wa Dodoma” alisema Senyamule.

Alisema shule zote zitakazopata mipira zitafuatiliwa na kuhakikisha inatumika vyema na kuwakilisha vizuri Mkoa katika michezo ya UMISETA kwa kufanya mazoezi kila siku kwasababu mipira ni bora na imara hivyo, isifungiwe bali itumike vyema.

Kwa upande wake Mwalimu Nestory Ngimbuzi, kutoka shule ya Msingi Fufu aliishukuru serikali kwa kutoa mipira ambayo itawasaidia watoto katika kuonesha vipaji vyao kwa sababu imekuwa ngumu kufuata ratiba ya michezo kutokana na ukosefu wa vifaa.

“Tunashukuru sana kwani imekuwa ni ndoto za wanafunzi wengi kukuza vipaji vyao. Michezo ni ajira hivyo, tunaamini mipira hii itakuwa chachu ya maendeleo ya sekta ya michezo kwa wanafunzi hapa Dodoma. Hapo mwanzo wanafunzi walikuwa wanatumia mipira ambayo wanatengeneza wenyewe kwa vitambaa na kamba kitu ambacho kilikuwa kinawafanya wasicheze kwa ufanisi” alisema Ngimbuzi.

Ikumbukwe kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya mageuzi katika sekta ya michezo ikiwemo kutoa hamasa kwa wachezaji wa timu ya Taifa na timu za Tanzania zinazoshiriki mashindano ya kimataifa pia ukarabati na ujenzi wa viwanja vipya vya michezo ikiwa ni katika harakati za kujiandaa na mashindano ya AFCON 2027.

Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE