WANAFUNZI WAIBA VITI VYA SHULE NA KUUZA
Wanafunzi watano wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Chuno, Manispaa ya Mtwara-Mikindani Mkoani Mtwara wamefukuzwa Shule kutokana na kuwa na tabia ya wizi wa kuiba viti vya Shule na kwenda kuviuza kama chuma chakavu.
Mkuu wa Shule hiyo, Hamisi Kaoneka, amesema tukio hilo la wizi limetokea March 7, 2024 usiku ambapo Wanafunzi hao walibainika wakibeba viti hivyo na kwenda kuviuza “Tukaenda mpaka kwenye eneo ambalo wanauza chuma chakavu ni maeneo ya Chuno uwanjani pale, kufika pale bahati nzuri ule muda nafika pale ndio walikuwa wanapakia kwenye lori, Wanafunzi hao sio mara ya kwanza kukabiliwa na kesi ya wizi, walishawahi kushitakiwa Shuleni kwa kuiba mabati mtaani na kwenda kuyauza kama chuma chakavu”
Mkuu huyo wa Shule amesema hayo wakati wa kikao cha Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Mwalimu Hassan Nyange na Viongozi wa elimu ngazi za Shule za Msingi na Sekondari , Watendaji wa Mitaa na Kata, Maofisa elimu na baadhi ya Wakuu wa Idara wa Manispaa hiyo kujadili mustakabali wa Sekta ya elimu.
Kwa upande wake Nyange ameelezea kusikitishwa na kitendo hicho “Sisi kama Manispaa tumejitahidi kwa kiasi kikubwa, mpaka sasahivi tumepeleka madawati zaidi ya 360 kwenye baadhi ya Shule ambazo watoto walikuwa wanakaa chini, kitu ambacho leo nimesema sitaki Mwanafunzi akae chini”
Comments