WAKULIMA WA ZABIBU DODOMA KUNUFAIKA NA UJENZI WA KIWANDA CHAMWINO

Wakulima wa zao la Zabibu kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino na Mkoa wa Dodoma kwa ujumla, wanatarajia kunufaika na kilimo cha zao hilo kufuatia ujenzi wa kiwanda cha kuchakata Zabibu kinachojengwa na Serikali kwenye Kata ya Chinangali 11 ambacho kitasaidia kuhifadhi zabibu iliyovunwa pamoja na mchuzi wake kwa ajili ya soko.

Hayo yamebainishwa leo Aprili 19, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alipofanya Mkutano wa hadhara na Wananchi wa Kata ya Mvumi Makulu katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kikazi pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Mkoa wa Dodoma.


Jawabu la ujenzi wa kiwanda hicho limefuatia kero iliyoulizwa na mwananchi juu ya ukosefu wa soko la zabibu. Mhe. Senyamule amesema Serikali sikivu ya awamu ya Sita inatambua umuhimu wa kilimo ndio maana inajenga kiwanda hicho ili kuwapunguzia adha wananchi wake kwa kupata uhakika wa soko. 


"Ujenzi wa kiwanda hiki unakuja kama mkombozi kwa Wakulima wa Zabibu kwa kuwa zabibu zitahifadhiwa pamoja na mchuzi wake kwa ajili ya kusubiri soko. Hii inatokana na Serikali yetu kufahamu kuwa asilimia 72 ya wananchi wanategemea kilimo ndio maana Mhe. Rais ametoa fedha zaidi ya Bilioni 90 hapa Chamwino kwa ajili ya kujenga mabwawa ya umwagiliaji ambayo yatasaidia kumwagilia ekari 8,000 kwa wakati mmoja" amesema Mhe. Senyamule 

Sanjari na Mkutano huo wa hadhara, Mkuu wa Mkoa ametembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali ikiwemo ujenzi wa barabara ya makutano ya Ntyuka - Mvumi - Makutano ya Kikombo (Km. 76) na Barabara ya Chololo - Mapinduzi (Makao Makuu ya TPDF - Km. 5).


Barabara hiyo inajengwa kwa awamu mbili (2), ambapo awamu ya kwanza ina urefu wa Km 25 na ya pili ni Km. 53. Jumla ya gharama za Mradi huo ambao umefadhiliwa na Serikali kuu kwa asilimia 100, unagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 38.199 na mpaka sasa utekelezaji wake umefikia 48% na unatarajiwa kukamilika June 2024.


Mradi mwingine uliotembelewa kwenye ziara hiyo ni Mradi wa ujenzi wa vyumba 7 vya Madarasa na matundu matatu ya vyoo kwenye shule ya sekondari Mvumi Mission iliyopo kwenye Kata ya Mvumi Mission.


Ujenzi wa Madarasa haya ambapo Matano yamekamilika na tayari yanatumika, mawili ndio yanaendelea na ujenzi pamoja na vyoo, unagharimu shilingi Milioni 145 na upo kwenye hatua za umaliziaji na pindi yatakapomalizika yatawezesha upatikanaji wa kidato cha Sita pamoja na kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani.


Aidha, Mradi wa Maji unaohusisha ujenzi wa tanki la kukusanya maji lenye ujazo wa Lita 50,000, Tanki la kuhifadhia maji ujazo wa Lita 200,000, mabomba ya kusambaza maji umbali wa Meta 14,399, vituo 16 vya kuchotea maji (DPs) vya malipo ya kabla unaendeleaje na unagharimu shilingi Milioni 988.8 huku utekelezaji wake ukifikia 77%.

Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE