MAMA AMTEKA MWANAE ILI MUMEWE AWALIPE MILIONI 20

 


WATU watatu akiwemo mama mzazi wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kula njama na kuficha mtoto ili baba wa mtoto huyo awalipe shilingi milioni 20 ili kumpata.


Watuhumiwa hao ni Wilfred Martin Komba, Agnes Jacob Mwalubuli (mama wa mtoto) na Hamida Gaudence Njuu wanaoendelea kushikiliwa kwa ajili ya kukamilisha taratibu zingine ili wafikishwe mahakamani.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime mtoto huyo wa kike mwenye umri wa miaka mitano, mwanafunzi wa shule ya awali ya Isaiah Samartan iliyopo Jijini Mbeya, alitoweka nyumbani kwao Mei 15, saa 11.45 jioni.

"Baada ya tukio hilo kuripotiwa polisi, baba mzazi wa mtoto, Layson Mkongwi, mfakanyakazi wa kampuni binafsi huko Jijini Mbeya alipokea simu kutoka kwa mtu asiyefahamika na kumweleza kuwa hatampata mtoto wake hadi atakapomtumia shilingi milioni ishirini," amesema Misime.

Amesema saa nne usiku wa kuamkia leo ndipo polisi walifanikiwa kumkamata Winfred, 36, ambaye ni Mngoni na Mkazi wa Vingunguti Dar es Salaam ambaye ndiye alikuwa akimpigia simu baba mzazi wa mtoto akimtishia kwamba asipotoa pesa hizo hatampata mtoto wake abadani.

"Baada ya kuhojiwa mtuhumiwa amesema walikula njama na mama mzazi wa huyo mtoto, Agnes, mkazi wa Isyesye Mbeya ya kujipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kwa baba mzazi wa mtoto. Aidha, ameeleza kuwa walifahamiana na mama huyo walipokuwa wakiishi katika nyumba moja ya kupanga huko Forest ya zamani Jijini Mbeya," amesema Kamanda Misime.

Kwa mujibu wa Misime, baada ya kupanga njama zao walifanikiwa kumchukuwa mtoto huyo na kwenda kumficha kwa rafiki yake aitwaye Hamida, anayeishi Jijini Mbeya.

Amesema ufuatiliaji ulifanyika na saa saba kasoro usiku wa kuamkia leo mtoto huyo alikutwa nyumbani kwa Hamida, huko Simike, Mbeya.

Amesema upatikanaji wa mtoto umechukuwa muda mrefu kutokana na kila ambalo polisi walikuwa wakipanga na kumshirikisha mama mzazi wa mtoto wakidhani ana uchungu na mtoto wake, yeye alikuwa akimfikishia taarifa mtuhumiwa mwenzake hivyo kufanya aendelee kukimbia kimbia na kujificha.

Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE