MKURUGENZI JIJI MATATANI KWA TUHUMA ZA RUSHWA



 Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha kuanza uchunguzi dhidi ya Mkurugenzi wa jiji la Arusha Mhandisi Juma Hamsini na baadhi ya wasaidizi wake wanaokabiliwa na tuhuma za rushwa na ubadhirifu wa fedha za walipa kodi.


Akizungumza na wadau wa utalii mkoani Arusha, Makonda amemuagiza Katibu Tawala wa mkoa huo Missaile Mussa kuwasimamisha kazi watumishi wote waliotajwa kuhusika na tuhuma hizo ili kupisha uchunguzi.

Makonda amechukua hatua hizo baada ya Mwenyekiti wa waongoza watalii Mkoa wa Arusha Wilbard Chambulo kudai kuwa baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha wamekuwa wakitengeneza nyaraka bandia pamoja na kuchepusha baadhi ya makusanyo ya kodi yanayotokana na sekta ya Utalii.

Chambulo amedai kuwa watumishi hao wamekuwa na kampuni hewa za utalii pamoja na kuwa na namba tofauti za ulipaji kodi na usajili hewa wa kampuni zenye kufanana na kampuni halisi za utalii zilizopo ndani ya Jiji la Arusha.

Mara baada ya malalamiko hayo Mkuu huyo wa Mkoa wa Arusha amesema Serikali yake inawajibikaji kuwa mlezi wa wafanyabiashara na wawekezaji wa mkoa huo, hivyo kamwe hatovumilia mtendaji yeyote anayekuwa sababu ya kukua kwa vitendo vya rushwa na kuua biashara.

Aidha Makonda amepiga marufuku halmashauri za mkoani Arusha kutumia Polisi kwenda kudai kodi kwa wafanyabiashara na kuagiza zitumike teknolojia zaidi kwenye kukumbusha na kudai madai mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

UDUMAVU BADO TISHIO -DUGANGE

SONGWE JOGGING WARUDI NA MEDANI ZAIDI YA KUMI NA TANO TULIA MARATHON

MOMBA HAWANA JAMBO DOGO: ROUTE VIONGOZI NA WANANCHI WAKUTANA PAMOJA ROUTER MATCH YANOGA