RC HOMERA AWAPA TANO TCCIA MBEYA AKIZINDUA MAONYESHO YA MBEYA CITY EXRO
Mkuu wa Mkoa wa mbeya Mhe. Juma Homera ameipongeza Taasisi ya Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoa wa Mbeya kwa ubunifu wa kuanzisha maonyesho ya biashara ya Mbeya City Expo
Pongezi hizo amezitoa leo Ijumaa Mei 24 , 2024 wakati akimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Ashatu Kijaji katika ufunguzi wa maonesho hayo yatayodumu kwa muda wa siku nane.
"Huu ni ubunifu mkubwa sana ambapo mmeweza kuwaalika mabalozi wa nchi jirani waje kujionea maonesho haya siku nyingine wasije peke yao waje na wafanyabiashara wao"
"Nichukue fursa hii kuwakaribisha mabalozi nchini Tanzania kutoka nchi ya Zambia, Zimbabwe, Malawi, DRC na Burundi" amesema
"Ili kuchochea ukuaji wa sekta viwanda na biashara nchini, Serikali inataka kusiwepo na Taasisi inayokuwa kikwazo kwa maendeleo ya sekta hiyo. Kama tunavyojua sekta binafsi zinachangia kwa kiasi kikubwa sana kutoa ajira kwa watanzania wengi hivyo kwa kuliona hilo ndio maana Serikali inahakikisha inaweka mazingira rafiki kwa sekta hiyo" amesema
Amewataka kuzifanyia kazi fursa zinazopatikana katika Mkoa wa Mbeya
"Rais Samia amefungua fursa za kibiashara na hapa juzi tulimuona Waziri wa Viwanda na Biashara amefanya Mkutano na watu wa sekta binafsi na wafanyabiashara hii ni kuhakikisha biashara hazikwami" amesema na kuongeza;
"Amewasihi wafanyabiashara pindi inapotokea changamoto suluhisho sio kufanya migomo zaidi ni kukaa mezani kutafuya suluhisho baina ya viongozi na wafanyabiashara. Kufanya migomo hakileti picha nzuri kwa mkoa na kwa taifa, matatizo husuluhishwa kwa mazungumzo" amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa wa Mbeya
Kwa upande wake rais wa TCCIA, Vincent Minja amesema kuwa kunafursa za kusafiri nje ya nchi wakati Rais Samia anapokwenda katika fursa za kibiashara hivyo kuwataka wadau hao kutumia fursa hiyo.
Comments