SILINDE AWAPA SIKU 30 WAMILIKI VIWANDA VYA CHAI KULIPA MADENI WAKULIMA
SERIKALI imetoa mwezi mmoja kwa wamiliki wa viwanda vya chai nchini kulipa madeni wanayodaiwa na wakulima wadogo wa zao hilo.
Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, alitoa agizo hilo juzi jijini hapa alipokuwa akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Chai Duniani.
"Hadi kufikia Juni 20 mwaka huu wamiliki wote wa viwanda wanaodaiwa na wakulima wadogo wa zao la chai wahakikishe wanalipa madeni hayo ili wakulima wetu wanufaike na kazi waliyofanya katika kipindi chote cha msimu,"alisema.
Aidha, Silinde alisema serikali imeweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa zao ilo kwa kufufua mashamba yaliyotelekezwa na kujenga viwanda saba vya kuchakata zao hilo vitakavyomilikiwa na wakulima wadogo.
Alisema mkakati mwingine wa serikali ni kuhakikisha inaweka miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba ya chai ili wakulima walime misimu yote.
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Chai Tanzania, Rukia Mwango alisema serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha zao la chai linasimama.
Alizitaja hatua hizo ni kutoa fedha kwa ajili ya kujenga viwanda saba vitakavyomilikiwa na wakulima wadogo, kutoa fedha kwa ajili ya kufufua mashamba ya chai ambayo yametelekezwa kwa muda mrefu.
Pia, alitaja changamoto zinazokabili zao la chai kuwa ni propaganda za baadhi ya watu ambazo zimechangia kudhoofisha soko la ndani la bidhaa hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chai Tanzania, Mustapha Umande, alisema lengo la kuadhimisha siku hiyo ni kutambua mchango wake katika kukuza ajira na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Alisema, serikali imeweka kipaumbele kuhakikisha sekta hiyo inakuwa kutokana na umuhimu wake hasa kiafya, kwamba husaidia kupungua athari za magonjwa ikiwamo kansa

Maoni