WAZAZI WALALAMIKA KUPEWA TAKA BAADA YA KUJIFUNGUA
Baadhi ya wanawake wanaojifungua katika Zahanati ya Leremeta iliyopo Kijiji cha Sinya, wilayani Longido, Arusha wanalazimika kupewa taka zitokanazo na uzazi wao ‘kondo’ kwa ajili ya kwenda kuziteketeza majumbani kwao.
Kukosekana kwa chemba ya kuchomeo taka kwa kituo hicho ni sababu ya wanawake hao kukutana na magumu hayo. Na kuna wakati wataalam wa afya hulazimika kuchimba shimo na kufukia taka za baadhi ya wazazi wanaokataa kuondoka nazo.
Utamaduni huo usiokubalika unaendelea katika kituo hicho kilichogharimu zaidi ya Sh88 milioni na kuanza kutoa huduma mwanzoni mwa mwaka huu na kina watoa huduma wawili ambao ni Ofisa Muuguza Msaidizi na Ofisa Tabibu.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Mei 23, 2024 na Ofisa Muuguzi Msaidizi wa Kituo hicho aliyejitambulisha kwa jina moja la Nurdeen, katika ziara ya siku ya kwanza ya Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda aliyoanza leo wilayani hapo.
“Changamoto kubwa inayotukabili hapa ni kutokuwa na chemba ya kuchomea taka zikiwemo taka za uzazi, hali inayotulazimu kuwapa baadhi ya wazazi wanaojifungulia kituoni hapa taka hizo kwa ajili ya kwenda kuziteketeza majumbani na wanaokataa kuondoka nazo tunazifukia kwenye mashimo,” amesema.
Picha iliotumika juu haihusiani na habari
Comments