MIAKA 120 JELA KWA UBAKAJI NA UNYANG'ANYI

Mahakama ya Wilaya ya Mbeya imemhukumu Samwel Mpese Kilundu kifungo cha miaka 120 Jela kwa makosa manne ambapo mtuhumiwa alihukumiwa kwa makosa mawili ya unyang'anyi wa kutumia silaha pamoja na makosa mawili ya ubakaji.


Akisoma hukumu hiyo, Hakimu wa Mahakama hiyo Mhe.Teddy Mlimba alisema kuwa mahakama imemtia hatiani mtuhumiwa baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha pasipo shaka tuhuma dhidi yake kwa makosa mawili ya unyang'anyi wa kutumia silaha chini ya kifungu cha 287 A cha Kanuni ya adhabu Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo 2022 na makosa mawili ya kubaka chini ya kifungu cha 130 (1) (2) (e) kanuni ya adhabu Sura ya 16 marejeo 2022, na hatimaye mtuhumiwa kupewa adhabu ya kutumikia kifungo Jela miaka 30 kwa kila kosa moja ambapo adhabu/ kifungo hicho kitakwenda sambamba.

Awali Mtuhumiwa alitenda makosa hayo yote mnamo Mei 11, 2023 huko maeneo ya Majengo mapya Jijini Mbeya ambapo alivamia nyumbani kwa mhanga na kunyang'anya vitu mbalimbali vikiwemo TV inch 55 na mali mbalimbali zote zikiwa na thamani ya Tshs. 6,245,000/=.

Aidha, siku ya tukio baada ya kufanya unyang'anyi huo, mtuhumiwa alimbaka msichana wa kazi [17] na mtoto wa mhanga [18] na kisha kuondoka.

Hata hivyo, Mtuhumiwa huyo amekuwa na historia ya kufungwa mara mbili, awali alihukumiwa kifungo jela kwa makosa ya kuvunja nyumba na kuiba mwaka 2017 na kufungwa Jela miaka 7, pia mwaka 2021 alitenda kosa la Wizi ambapo kifungo chake kilimalizika tarehe 28/01/2023.

Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE