MKURUGENZI AAGIZWA KUWANUNULIA VISHIKWAMBI MADIWANI

 


Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Kighoma Malima amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo kuwanunulia madiwani wa halmashauri hiyo vishkwambi kwa lengo la kupunguza gharama na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi zao.

Malima amebainisha hayo wakati wa mkutano maalum wa Baraza la Madiwani kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali – CAG kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya wilaya hiyo.

Malima amesema madiwani wanapaswa kuwa na simu hizo ambazo zitawawezesha kutekeleza majukumu yao ya kazi kwa haraka na kwa ufanisi hivyo kuongeza kasi ya utendaji kazi. Kwa sababu hiyo ameagiza vishikwambi vya madiwani hao viwe vimekwishanunuliwa kabla au ifakapo Septemba 30, 2024 ambavyo pamoja na kazi nyingine vitasaidia kupunguza gharama ya kununua karatasi kwa ajili ya vikao.

“Kabla ya tarehe 30 mwezi wa tisa kikao chochote cha madiwani kitakachofanyika baada ya hapo lazima madiwani wawe na vishikwambi,” amesema Malima.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Jabir Makame amesema halmshauri hiyo imeweza kujikita katika sekta ya kilimo ili kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ambapo hadi sasa miche elfu 40 ya zao la parachichi tayari imeshapandwa kupitia miradi mbalimbali huku halmashauri hiyo ikiwa imejipanga kuzalisha miche elfu 80 na ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wilaya itakuwa na jumla ya miche isiyopungua 240,000.

Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ali Mussa amesema, Halmashauri ya Wilaya ya Gairo imepunguza ukusanyaji wake wa mapato ukilinganisha na siku za nyuma na kuwataka kujitathmini na kuangalia namna bora ya kukusanya mapato hayo kwa lengo kuwaletea Wanagairo maendeleo, Mkoa na Taifa kwa jumla.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mussa ameitaka Halmashauri hiyo kupeleka banki fedha zote za makusanyo ya ndani wanazokusanya na kuzikumbusha halmashauri zote za mkoa huo kuwa mwisho wa kupeleka fedha hizo benki ni tarehe 30 Juni 2024 ili kuepusha fedha hizo kutumika zikiwa bado hazijaingizwa kwenye mifumo ya serikali.

Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE