NFRA YAKABIDHIWA SUKARI SASA KUANZA KUNUNUA NA KUHIFADHI KUKABILIANA NA UHABA WA SUKARI

 

Dk. Mwigulu Nchemba  Waziri wa fedha amesema NFRA, inakwenda kutibu shida ya kupanda mara kwa mara kwa bei ya sukari nchini hali ambayo imekuwa ikiibua maswali na malalamiko kutoka kwa wananchi.

"Tunakwenda kuanza kuitumia NFRA kununua sukari na kuhifadhi kama ambavyo imesaidia katika kuhifadhi mazao mengine ya chakula," amesema Dk. Mwigulu. 

Aidha, amesema NFRA inatumika kutokana na kufanya vizuri katika kuhifadhi mazao mengine kwa ajili ya usalama wa chakula.

"Kesho nitasoma muswada wa sheria ya fedha ambao hapa bungeni utakwenda kuruhusu kutumika kwa NFRA kununua na kuhifadhi sukari kuanzia mwaka mpya wa fedha na hii itakwenda kutibu upandaji wa bei ya sukari holela," amesema.

Amesema, serikali hutoa msamaha wa kodi na tozo katika bidhaa mbalimbali nchini, lakini hali hiyo imekuwa haiwanufaishi wananchi wa kawaida na badala yake wameitumia fursa hiyo kwa maslahi yao binafsi.

"Tumetoa msamaha kwenye taulo za kike hakuna kilicho badilika, tumetoa ruzuku ya mafuta wananchi hawajanufaika chochote wafanyabiashara wamechukua hii kama fursa kwao kujinufaisha wenyewe kwa maslahi yao binafsi hivyo tunakwenda kuanza kutumia NFRA kununua na kuhifadhi sukari kama ambavyo tumefanya katika mazao mengine ili kutibu tatizo la sukari," amesema.

Aidha, amesema moja ya hoja iliyoibuliwa na wabunge wakati wa kuchangia mjadala wa bajeti kuu ni suala la malipo ya makandarasi.

Dk. Mwigulu, alisema katika kipindi kirefu makandarasi nchini wamekuwa wakidai malipo ya miradi waliyotekeleza kwa muda mrefu hali iliyosababisha kuongezeka kwa madai hayo mwaka hadi mwaka.

“Kweli madeni haya yalikuwa ya muda mrefu sana na kuna makandarasi ambao walikuwa hawajui watalipwa lini madai yao, lakini tuishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye kwa kiasi kikubwa amelipa madai hayo.

“Lakini serikali tutaendelea kuhakikisha malipo haya yanalipwa kwa wakati kwa makandarasi wote wanaotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo,” amesema.

Kuhusu hoja ya matumizi ya gesi asilia kwenye magari ya serikali, Mwigulu amesema watakuwa mfano katika matumizi ya nishati hiyo.

“Sisi serikali tunakwenda kuwa mafano wa matumizi ya nishati ya gesi asilia kwenye magari ya serikali tutakwenda kuanzisha kituo cha ujazaji wa gesi kwenye magari katika mikoa ya Dodoma, Morogoro na Dar es Saalam na maeneo mengine,” amesema.  

Kuhusu malalamiko ya wafanyabiashara mambo mbalimbali ambayo yamekuwa kero kwao, Dk. Mwigulu amesema hakuna haja ya kugoma kwa kuwa serikali ya awamu ya sita ni sikivu na kila walicho kilalamikia kitafanyiwa kazi.

“Hatuna sababu ya kufika huko tunarudishana nyuma, serikali hii sikivu imesikia kilio cha wafanyabiashara na kila hoja yao itafanyiwa kazi kama ambavyo mambo mengine tumeyashughulikia,” amesema.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema serikali inaendelea na jitihada za kuongeza uzalishaji wa bidhaa zinazotumika kwa wingi nchini ili kupunguza uagizaji kutoa nje ya nchi.

“Bidhaa hizi ni pamoja na mafuta ya kula, ngano mazao  ya chakula, dawa mavazi na kadhalika pia tunaendelea kulinda uwekezaji unaochochea uwekezaji nchini,” amesema.

Amesema lengo la serikali ni kujitosheleza kwa sukari na kuondokana na shida ya ‘Gap Sugar’ kwa kuwekeza katika sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mazao ambayo yatatumiwa na viwanda vya ndani kuzalisha bidhaa hiyo.

“Tuachane watu ambao wanasema serikali ina nia ya kuua viwanda vya ndai vya sukari kama tungekuwa tunataka kuua basi tusinge samehe kodi ya Sh. bilioni 240 kwa viwanda vya ndani vinavyozalisha sukari ili kuvijengea uwezo,” amesema Prof. Mkumbo.



Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE