RUTO AUKATAA MUSWADA ULIOLETA MACHAFUKO
RAIS wa Kenya, William Ruto amekataa kutia saini muswada ulio na utata wa fedha wa mwaka 2024, uliosababisha maandamano na vurugu nchini humo. Ruto ameurejesha tena mswada huo bungeni ili ufanyiwe marekebisho.
Taarifa hiyo imekuja baada waandamanaji nchini humo wakiapa kuendelea na maandamano yao kupinga nyongeza mpya za ushuru, siku moja tu baada ya polisi kufyatua risasi na kusababisha mauaji ya watu kadhaa katika maandamano hayo yaliyogeuka kuwa vurugu.
Rais William Ruto sasa anatarajiwa wakati wowote kutoka sasa kulihutubia taifa kufuatia maandamano ya kuupinga mswada huo.
Hatua hii inakuja baada ya Bunge la Kenya kuidhinisha vikosi vya jeshi la KDF kulinda usalama vikishirikiana na polisi wa Kenya kufuatia purukushani zinazoendelea nchini humo. Bunge kwa sasa limeenda likizo hadi Julai 23 mwezi ujao.
DW imeripoti kuwa, Spika wa Bunge la nchi hiyo, Moses Wetangula amewasifu vijana kwa ujasiri wao ila amesisitiza kwamba malalamiko lazima yafuate mkondo wa sheria ndipo yapate kusikilizwa. Kadhalika mahakama ya Eldoret imesitisha operesheni kwa muda baada ya waandamanaji kuharibu hati muhimu hapo jana.
Bado waandamanaji wanajipanga kumiminika barabarani tena kesho Alhamisi Juni 27, 2024 kuendelea na mapambano ya kuupinga mswada huo.
Comments