UPATIKANAJI WA MAJI KIBAHA ASILIMIA 78

HALI ya upatikanaji wa maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kwa sasa ni asilimia 78 huku malengo yakiwa kufika asilimia 85 ifikapo Disemba, 2025.


Kiwango hicho kimefikiwa kutokana na miradi mbalimbali inayotekelezwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kibaha, Mhandisi Debora Kanyika amebainisha hayo alipokuwa alitoa taarifa yake kwenye Baraza la Madiwani lililofanyika katika Halmashauri hiyo kwa ajili ya kupokea taarifa ya miradi inayotekelezwa na taasisi hiyo.



Mhandisi Debora amesema hali ya upatikanaji wa maji imeongezeka hadi asilimia 78 kutoka asilimia 67.5 mwaka 2019 kulingana na miradi inayoendelea kutekelezwa.

Hata hivyo, meneja huyo amesema bado kuna upungufu wa maji kwenye maeneo ya Vijijini, hususan Kata ya Gwata na katika maeneo ya Dutumi ambapo ipo miradi inalengwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 ili kumaliza changamoto hiyo.

Kwa mujibu wa Mhandisi Debora, katika bajeti ya mwaka 2024, utekelezaji wa miradi umelenga kutumia Shilingi Bilioni 1.7; na hadi sasa, fedha zilizotumwa za P4R Shilingi Bilioni 1.6. Bajeti hiyo imejikita katika kukamilisha miradi inayoendelea ya Kwala, Ruvu Stesheni pamoja na kukarabati vituo vya maji.

Pia, Mhandisi Debora amesema changamoto wanayokabiliana nayo kwa sasa ni pamoja na ongezeko la watu ambalo limesababishwa na ujenzi wa viwanda na makazi ya kisasa; hata hivyo, Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kukabiliana na hali hiyo.

Katika kikao hicho, Madiwani walimpongeza Meneja wa RUWASA wa Wilaya ya Kibaha kutokana na ushirikiano anaowapatia pale inapohitajika katika utekelezaji wa majukumu yake ya kuwaunganishia wananchi huduma ya maji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Erasto Makala amesisitiza taasisi hiyo kuendelea kutekeleza miradi kwa bidii Ili kuwaondolea Wananchi changamoto ya kutumia muda mwingi kutafuta maji.

Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE