WATATU WAFARIKI KWA AJALI MAKETE
Watu watatu wamefariki dunia wilayani Makete mkoani Njombe kwa ajali ya lori lenye namba za usajili T 911 BHX lililokuwa limebeba viazi baada ya lori hilo kuacha barabara na kupindukia mtoni katika eneo la Kilanzi darajani kijiji cha Ndulamo
Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe Mahamoud Banga amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambapo amesema imetokea Juni 27,2024 majira ya saa mbili asubuhi baada ya gari hilo kumshinda dereva na kuwataja waliofariki dunia kuwa ni Yohana Mkemanga miaka 35 (dereva), Mussa Sanga (kondakta) na Hamza mkazi wa Morogoro aliyebebwa kama abiria
Daktari Vitusi Paul ni Mganga Mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Makete akizungumza na Green Fm amesema wamepokea miili ya marehemu na kuwataka ndugu zao kufika hospitalini hapo kuwatambua marehemu.
Keneth Kidumage mkazi wa Usalule wilayani Wanging'ombe ni dalali ya viazi vilivyokuwa vimebebwa na lori hilo amesema mzigo huo wa viazi maroba 210 ameubeba kutoka kata ya Bulongwa na Iniho na ulikuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni kumi na moja
Kuhusu kama Dereva alikuwa ametumia kilevi kabla ya safari, Kidumange amekanusha suala hilo huku akielezea kuwa amelazimika kuokoteza viazi hivyo na anachokishubiri ni kuzungumza na mmiliki wa gari kuona namna ya kusaidiana juu ya hasara iliyojitokeza
Comments