KATIBU MKUU NISHATI AWATAKA TANESCO KULEGEZA BEI YA UMEME ILI WANANCHI WAPIKIE NISHATI YA UMEME
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) sanjari na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kulegeza bei ya umeme, ili mwananchi asiogope kupikia umeme badala ya nishati nyingine.
Akiwa katika ziara yake kutembelea Banda la Wizara ya Nishati sambamba na mashirika na taasisi zilizo chini yake katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba 2024) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, vilivyopo Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam, Mramba amesema ni lazima wananchi wawe na machaguo mengi ya aina ya nishati wanayotaka kupikia ima umeme, gesi ama mkaa.
“Umeme ndio nishati safi zaidi kulinganisha na nishati nyingine kama gesi na mkaa, lakini ili mwananchi aweze kutumia umeme ni lazima umeme uwe wa bei nafuu,
“Kinachonisumbua ni kwamba mwananchi anakuwa na umeme nyumbani lakini umeme sio chaguo lake la kupikia, hii sio sahihi, Mfano watu wengi wa Dar es Salaam wana umeme, nilitaka wawe na uwezo wa kutumia umeme kupikia,” amesisitiza.
Amesema, umeme unapaswa kuwa nafuu kwa Watanzania wa mijini na vijijini kwa kuwa hivi sasa maeneo mengi ya nchi tayari wananchi wameunganishwa na nishati ya umeme
Amewataka TANESCO na REA kuondoa ile dhana ya kuwa umeme ni ghali, kwa kuwa hicho ndicho kinachowafanya wananchi kukimbilia gesi na mkaa kama machaguo yao ya kupikia badala ya umeme ambao ni salama zaidi.
Katika ziara hiyo, Katibu huyo amevutiwa na ubunifu unaotumika katika kutengeneza jiko la umeme la ‘positive cooker’ maarufu jiko janja kwakuwa linatumia kiasi cha unit 1 ya umeme kwa saa lakini ni jiko ambalo halina mitetemo ya umeme wala ‘kupiga shoti’.
“Nawapongeza TANESCO kwa ubunifu huu (wa jiko janja ‘positive cooker’) lakini tafiti sokoni zinaendelea na ndio maana kila siku teknolojia inabadilika,” ameagiza Katibu Mkuu.
Comments