MAAFISA ARDHI ILEMELA MATATANI KWA TUHUMA ZA RUSHWA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani humo kuwakamata Mkuu wa Idara ya Ardhi wa Manispaa ya Ilemela Grace Masawe pamoja na Afisa Mipango Miji Mwajuma Mabula kwa tuhuma za kuomba Rushwa.
Mhe. Mtanda ametoa agizo hilo leo tarehe 16 Julai, 2024 Mtaa wa Igoma kwenye Mkutano wa kusikiliza na Kutatua kero za wananchi na ndugu Matiko Migire kuwasilisha kero kwamba watumishi hao wamemuomba rushwa ya Tshs. 2,430,000 ili wafanye upimaji wa viwanja na. 311, 312 na 313 Block A Pasiansi.
Mhe. Mtanda amesema kitendo hicho si cha kiungwana na kinawanyima haki wananchi hivyo wakati TAKUKURU wanalichunguza suala hilo Idara ya ardhi amewapa siku saba kukamilisha Upimaji wa viwanja hivyo kwani wamemzungusha kwa muda mrefu mteja huyo anayefuatilia bila mafanikio.
Awali, akiwasilisha kero hiyo kwa Mkuu wa Mkoa, Matiko alifafanua kuwa 2019 Halmashauri hiyo iliomba Hati za viwanja hivyo na kuzifuta na kuahidi kufanya upimaji mwingine na kuwataka wamiliki Joseph Mashiku, Hezeline Chawachi na Desderius Ntobi kwa gharama ya 500,000 ambayo wametoa namba ya kulipia.
Ameendelea kusema kwamba Idara hiyo ya Ardhi haijawahi kutekeleza ahadi yao kwenye viwanja hivyo na badala yake wamekua wakimtafuta kwa simu kupitia mtuhumiwa Mwajuma na kumtaka atume kwenye kiasi hicho (2,430,000) ikiwa fedha halali anayotakiwa kulipia huduma ni Tshs. 500,000 tu.
Akizungumzia kero ya Maji kwenye baadhi ya Mitaa ya Nyamagana, Mhe. Mtanda amesema kupitia Mkopo wenye masharti nafuu wa Tshs. Bilioni 400 kutoka Shirika la Maendeleo la Ufarasa (AFD) Mamlaka ya Maji (MWAUWASA) itasambaza Maji kwenye umbali wa zaidi ya Kilomita 700 kutoka Chanzo cha Butimba na watamaliza kero kwa wananchi wengi.
Comments