SILINDE AFANYA ZIARA IRINGA YA UKAGUZI
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) amekagua kituo cha Seatondale kinachosimamiwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kwenye kituo cha Kifyulilo kilichopo Iringa mjini na kukagua Kampuni ya Chilongola Agro Forest and Livestock Limited iliyopo Mafinga, Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa ambalo ni shamba la vijana wanaojihusisha na uzalishaji wa miche bora ya parachichi.
Ziara hiyo imefanyika tarehe 6 Julai 2024 ikiwa ni maandalizi ya kumpokea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) ambaye atatembelea maeneo hayo tarehe 7 Julai 2024.
Kituo cha Seatondale ni miongoni mwa vituo vidogo vinavyotumika kufanyia majaribio ya mazao ya kilimo kutoka vituo vingine vya utafiti vya TARI pamoja na wadau wengine wa Sekta ya Kilimo. Kituo cha Seatondale kipo katika ukanda wa futi 5,463 (mita 1,665) toka usawa wa bahari na kinapokea mvua za wastani wa milimita 800 kwa mwaka.
Aidha, Kituo kina jumla ya hekta 11.2 (sawa na ekari 28). Hekta 5.2 zinatumika kwa shughuli za majaribio pamoja na majengo; wakati hekta 6 ziko kwenye mpango kazi wa kuanzisha bustani ya parachichi na kilimo cha mboga mboga na matunda
Comments