WANANCHI WAMETAKIWA KUITUMIA VIZURI MITANDAO YA KIJAMII

 


WANANCHI wametakiwa kutumia vizuri mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na kuepuka kuweka taarifa zao za siri ili zisidukuliwe na watu wenye nia ovu na wakazitumia kwenye matukio ya uhalifu.


Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Tekonojia ya Habari, Maryprisca Mahundi, alitoa wito huo mwishoni mwa wiki alipozungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mbeya (CUoM) pamoja na wahadhiri.


Alisema baadhi ya watu wamekuwa wakidukua taarifa muhimu za watu wengine kwenye mitandao na kuzitumia kukopa fedha kwenye taasisi zinazokopesha kupitia mitandao na kuwaweka wahusika kama wadhamini.


Alisema wanaposhindwa kurejesha mikopo hiyo ndipo taasisi hizo zinaibuka na kuanza kutuma jumbe zenye vitisho na hapo ndipo wahusika wanaanza kushtuka na kulalamika bila kujua kwamba walisababisha wao wenyewe kwa kuweka taarifa zao muhimu mitandaoni.


“Hivi karibuni Rais Samia alituzindulia taasisi ya kulinda taarifa binafsi, lakini bado kuna watu ni watundu huko kwenye mitandao, wanaweza kuchukua taarifa zako na kuzitumia vibaya, jitahidi usiweke taarifa zako muhimu huko,” alisema Mahundi.


Makamu Mkuu wa CUoM, Prof. Romuald Haule alisema waliandaa kongamano maalumu la kuadhimisha mwaka mmoja wa chuo hicho tangu kilipopanda hadhi.


Alisema lengo la kongamano hilo ni watumishi pamoja na wanafunzi kutafakari maendeleo yao waliyoyapata katika kipindi cha mwaka mmoja na malengo ya mwaka unaofuata.

Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE