WAZAZI WAMETAHADHALISHWA KUWA KARIBU NA WATOTO WAO
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Theopista Mallya ametoa tahadhali kwa wananchi kuhusiana na taarifa zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba watoto wanatekwa kwa kuwaambia wananchi wote kuendelea kuwa karibu na watoto wao na kuhakikisha wanafahamu watoto wao walipo ili kuwafanya kuwa salama wakati wote.
Ameyasema hayo Julai 23, 2024 alipokuwa anaongea na waandishi wa habari ofisini kwake na kusema alipokea taarifa kutoka kwa Kondakta wa basi la AM Safari linalofanya safari zake kutoka Kigoma kwenda Dodoma hadi Dar es Salaam kwamba kuna mtoto ametelekezwa kwenye basi hili aitwaye Lightness Taifa (3) na jitihada za kuwatafuta wazazi wake zimefanyika kuweza kumkabidhi mtoto huyo.
"Mtoto huyo alipotea katika mazingira ambayo mama wa mtoto alienda kumtafutia chips mtoto wake na baada ya kurudi hakumkuta kumbe mtoto huyo alimfuata mama yake bila ya mama yake kujua na ndipo alipopotea hadi alipokuja kupatikana kwenye basi la AM Safari akiwa hana mtu aliyeambatana naye na ndipo kondakta wa basi hilo alipotoa taarifa Polisi kwa ajili ya kupatiwa msaada mtoto huyo" amesema Kamanda Mallya.
Kwa upande wake mama wa mtoto huyo Ester Antony (24) amethibitisha kupatikana kwa mtoto wake na amelishikuru Jeshi la Polisi kwa jitihada za kumpata mtoto huyo kwani alipotea Julai 13, 2024 na amepatikana Julai 17, 2024 akiwa kwenye basi la AM Safari Jijini Dodoma.
Comments