WATIA NIA WANAOTUMIA MISIBA KUPATA UMAARUFU WAONYWA
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Salim Abri Asas, amesema baadhi ya watia nia katika wilaya ya Iringa Vijijini wamekuwa wakitumia mbinu zisizo za kimaadili, kama vile kuomba misiba itokee ili wapambe wao wapate nafasi ya kutoa rambirambi na kujipatia umaarufu wa kisiasa.
Akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilaya ya Iringa Vijijini, Asas amesema kuwa baadhi ya wagombea wamekuwa wakiwatumia wapambe wao kupeleka rambirambi kwenye misiba hiyo akionya hali hiyo kuwa inakiuka kanuni za chama cha mapinduzi CCM, ambazo zinahitaji utaratibu wa haki katika upatikanaji wa nafasi za uongozi lakini inatengeneza makundi yasiyo na afya ndani ya chama.
ASAS amesema wapambe hao wanashindwa kujihusisha katika kusaidia jamii kwenye changamoto mbalimbali kama afya, elimu, miundombinu na badala yake wanatafuta misiba kujijenga kisiasa akionya kwamba watakapokatwa waendelee kusaidia jamii na sio kuisaidia jamii katika kipindi hiki tu cha kusaka uongozi.
Hatahivyo Asas amesema wilaya hiyo inatajwa kuwa na wapambe wengi ambao wanagawana wagombea kulingana na ushindani wa upambe, hali inayohitaji marekebisho ili kuhakikisha taratibu sahihi zinazingatiwa.
MNEC Asas anaendelea na ziara yake ya kuzungumza na wajumbe wa Halmashauri za wilaya, ambapo tayari ametembelea wilaya za Mufindi, Kilolo, na Iringa Vijijini akitarajiwa kumaliza ziara yake wilaya ya iringa mjini
Comments