MKUU WA MKOA WA SONGWE ZIARANI TUNDUMA
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Daniel Chongolo, amefanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Mji Tunduma mnamo tarehe 24 Septemba 2024. Ziara hiyo iliangazia kutatua changamoto za wananchi na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo. Akiwa katika mkutano wa hadhara, Mhe. Chongolo alisikiliza na kutoa ufumbuzi wa kero mbalimbali, akisisitiza ushirikiano kati ya serikali na wananchi katika kuboresha huduma za kijamii.
Miongoni mwa miradi aliyotembelea ni kituo cha afya cha Chiwezi, ambacho kinajengwa kwa gharama ya zaidi ya Shilingi milioni 786. Kati ya fedha hizo, milioni 500 zimetolewa na serikali kuu, milioni 286 zimetokana na mapato ya ndani, na milioni 8 zimetokana na nguvu za wananchi. Ujenzi wa kituo hicho unajumuisha majengo ya huduma muhimu kama maabara, upasuaji, wodi ya mama na mtoto, chumba cha kufulia nguo, na chumba cha kuhifadhi maiti, pamoja na njia za kupitisha wagonjwa. Kituo hiki kitahudumia wakazi 10,540 wa Kata ya Chiwezi pamoja na maeneo jirani kama Kata ya Chindi (Halmashauri ya Momba) na Kata ya Ipunga (Halmashauri ya Mbozi), hivyo kupunguza umbali wa kufuata huduma za afya hadi Hospitali ya Mji wa Tunduma.
Aidha, Mhe. Chongolo alikagua maendeleo ya ujenzi wa daraja kubwa linalounganisha Halmashauri ya Wilaya ya Momba na Halmashauri ya Mji Tunduma, mradi wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 2.9 Hadi sasa, mradi huo umefikia asilimia 40 ya utekelezaji, ukigharimu Shilingi bilioni 1.2, na unatarajiwa kukamilika Oktoba 2025. Mkuu wa Mkoa alimhimiza mkandarasi kuongeza kasi ili daraja hilo likamilike mapema, kwani litasaidia katika kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa pande zote mbili.
Ziara ya Mhe. Chongolo imeibua matumaini makubwa kwa wakazi wa Tunduma na maeneo jirani, hasa kutokana na umuhimu wa miradi hiyo katika kuboresha huduma za afya, miundombinu, na kuinua uchumi wa mkoa wa Songwe.
Comments