SONGWE:VITONGOJI 90 KUANZA KUNUFAIKA NA UMEME WA REA,BILIONI 10.8.ZATOLEWA
Katika juhudi za kuboresha huduma za nishati vijijini, serikali imetenga shilingi bilioni 10.8 kwa ajili ya mradi mkubwa wa kusambaza umeme katika vitongoji 90 vilivyopo ndani ya majimbo sita ya Mkoa wa Songwe. Mradi huu unalenga kuinua hali ya maisha kwa wakazi wa maeneo hayo kwa kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Daniel Chongolo, wakati wa hafla fupi ya utambulisho wa Mkandarasi aliyepata jukumu la kutekeleza mradi huo. Hafla hiyo iliofanyika Septemba 26, 2024, katika ofisi za mkoa, ambapo kampuni ya China Railway Construction Electrification Bureau Group Co. Ltd kutoka nchini China ilizinduliwa rasmi kama mtekelezaji wa mradi huo.
Mhe. Chongolo alibainisha kuwa mradi huo ni sehemu ya awamu ya tatu ya Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA), unaoendelea kutekelezwa na serikali kwa lengo la kuongeza wigo wa upatikanaji wa umeme katika maeneo ambayo hayajafikiwa na nishati hiyo. "Huu ni mradi muhimu ambao utafungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wetu, hasa katika vitongoji ambavyo vimekuwa na changamoto ya upatikanaji wa umeme kwa muda mrefu," alisema Chongolo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, zaidi ya kaya elfu kumi na tano zinatarajiwa kunufaika moja kwa moja na mradi huu mara tu utakapokamilika. "Tunatarajia ukuaji wa shughuli za uzalishaji mali kama vile viwanda vidogo vidogo na biashara za huduma, jambo ambalo litaongeza kipato cha wananchi na kuchangia uchumi wa mkoa wetu," aliongeza.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa kampuni ya China Railway Construction Electrification Bureau Group Co. Ltd aliahidi kutekeleza mradi huo kwa ufanisi na ndani ya muda uliopangwa, akisema kampuni yao ina uzoefu mkubwa katika miradi ya aina hii katika nchi mbalimbali.
Mradi huu wa umeme unakuja wakati ambapo Mkoa wa Songwe unashuhudia ongezeko la uwekezaji katika sekta mbalimbali. Kwa miaka ya karibuni, serikali imekuwa ikihamasisha uwekezaji kwenye viwanda, kilimo, na miundombinu, na sasa upatikanaji wa umeme unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo hayo.
Wakazi wa vitongoji vinavyotarajiwa kunufaika na mradi huu wameonesha furaha yao, wakisema kuwa upatikanaji wa umeme utaondoa changamoto za muda mrefu walizokuwa wakikabiliana nazo, ikiwemo gharama kubwa za nishati mbadala na kukosekana kwa huduma bora za kijamii kama vile afya na elimu.
Mradi wa REA unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mkoani Songwe unathibitisha dhamira ya serikali katika kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata huduma muhimu za nishati kwa ajili ya kuboresha maisha yao. Kadiri mradi unavyosonga mbele, matarajio ni kuona mabadiliko makubwa katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi ndani ya Mkoa wa Songwe
Comments