RC CHONGOLO AMETEMBELEA MRADI WA MAEGESHO YA MAGARI YA MIZIGO CHIMBUYA,MBOZI
Songwe, Tanzania – Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Daniel Chongolo, amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha maegesho ya magari ya mizigo (malori) katika eneo la Chimbuya, Wilaya ya Mbozi. Mradi huu ni sehemu ya juhudi za serikali za kuboresha miundombinu ya uchukuzi na kurahisisha usafirishaji wa mizigo katika maeneo yanayopakana na mipaka, hususan mpaka wa Tunduma.
Mradi huo unatekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na unaendelea chini ya usimamizi wa mkandarasi Mehrab Construction Co. Ltd. Kituo hicho kitakapokamilika, kitakuwa na uwezo wa kupokea malori takribani 90 kwa wakati mmoja, hatua ambayo itasaidia kupunguza msongamano wa magari katika barabara za mipakani, ambapo mara nyingi malori yanakuwa yameegeshwa kiholela kando ya barabara.
Mhe. Chongolo, akiwa na viongozi wa Mkoa, alisisitiza umuhimu wa kukamilisha mradi huo kwa wakati uliopangwa ili kuanza kutoa huduma haraka kwa manufaa ya wafanyabiashara na wananchi wa Songwe na maeneo ya jirani. "Mradi huu ni muhimu kwa ukuaji wa kiuchumi wa mkoa na unatarajiwa pia kuleta faida kubwa katika kudhibiti uharibifu wa barabara na kuongeza usalama wa magari na abiria," alisema Chongolo.
Kaimu Meneja wa Tanroads Mkoa wa Songwe, Eng. Silvan Mloka, alieleza kuwa ujenzi wa kituo hiki ni hatua muhimu katika kuimarisha uchumi wa eneo hilo. Aliongeza kuwa kituo hicho kitakuwa chanzo cha mapato ya ndani kwa Tanroads Songwe na kitasaidia kuboresha matumizi ya barabara kuu kwa kupunguza msongamano wa magari makubwa kwenye barabara.
Kwa mujibu wa Eng. Mloka, mradi unakadiriwa kugharimu zaidi ya Sh1.86 bilioni na unatarajiwa kukamilika mapema mwaka ujao. Alisema, "Lengo ni kuhakikisha kwamba magari hayaleti tena msongamano barabarani na barabara haziharibiwi kwa kuwa na malori mengi yaliyosimama pembezoni. Mradi huu ni suluhisho endelevu la changamoto hii."
Kituo hiki kitakamilisha mabadiliko makubwa katika miundombinu ya mkoa, hasa kwa wafanyabiashara na wasafirishaji wa mizigo wanaoingia na kutoka Tanzania kupitia mipaka ya Tunduma na Zambia.
Comments