WAACHIWA HURU KESI YA MAUAJI BAADA YA MIAKA 10,NDUGU WAAGUA KILIO



Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es salaam imewaachia huru Vijana Watatu wa Kitanzania Baraka Machange, Yasin Omary na Ally Said maarufu BabuAli waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya Mtoto wa miaka nane aitwaye Glory Tumaini Metta katika kesi ambayo imeunguruma kwa miaka 10 tangu 2014 wakidaiwa kutenda tukio hilo October 10, 2014 maeneo ya Kimara Temboni Dar es salaam.


Ilikua ni furaha Mahakamani hapo baada ya Vijana hao kuachiwa lakini ilikua ni huzuni na vilio kwa Baba na Mama mzazi wa Marehemu Glory baada ya Jaji Elizabeth Mkwizu kusema Mahakama hiyo inawaachia huru Washtakiwa hao kutokana na upande Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao.


Jaji Mkwizu alisema baada ya Mahakama kupitia ushahidi wa pande zote mbili ilijiuliza maswali kadha wa kadha ikiwemo ni nani aliyewaona Watu hao wakifanya mauaji lakini pia Mahakama haikuelezwa namna vielelezo mbalimbali vilivyohifadhiwa ama kupewa namba ikiwemo tofali, mchanga na nguo zilizokutwa eneo la tukio.


Jaji huyo alisema pia Mahakama haikuelezwa jinsi vipimo vya damu vya Mshtakiwa namba moja, Marehemu Glory na Mama Mzazi wa Marehemu namna vilivyohifadhiwa ama kupewa lebo hadi kufikishwa Mahakamani.


Vijana hao watatu inadaiwa siku ya tukio October 10 2014 walimchukua Mtoto huyo kwenda kumbaka na kumuua na ilisemekana kuwa walimpiga na kitu kizito ( kinachodhaniwa kuwa tofali) ambapo mashtaka haya yalifanya washikiliwe Mahabusu kwa takriban miaka kumi hadi leo walipoachiwa huru

Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE