AGIZO LA WAZIRI WA UJENZI LATEKELEZWA KWA VITENDO SONGWE
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imetekeleza kwa mafanikio maagizo ya Wizara ya Ujenzi yanayolenga kupunguza changamoto ya msongamano katika barabara ya TANZAM, hususan eneo la Tunduma, maagizo ambayo yalitolewa Novemba 18, 2024 na Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Innocent
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Songwe, Mhandisi Suleiman Bishanga, amesema juhudi hizo ni matokeo ya mwongozo uliotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Innocent Bashungwa.
"Waziri alitoa maagizo ya kutafuta suluhisho la haraka, na kwa kushirikiana na TANROADS Mkoa wa Mbeya, tumefanikisha kupunguza msongamano mkubwa uliokuwa ukisababisha usumbufu kwa madereva," alisema Mhandisi Bishanga.
Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuweka mizani ya ziada inayohamishika (mobile weighbridge) kwa ajili ya kupima magari yanayotoka Tunduma kwenda Dar es Salaam, uimarishaji wa usimamizi wa magari kupitia mfumo wa mizani ya kupima magari yakiwa kwenye mwendo (weigh in motion) na kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha magari yanayosubiri huduma hayakai kwa muda mrefu.
Aidha Mhandisi Bishanga amesema, ujenzi wa maegesho mapya katika eneo la Chimbuya unaendelea kwa kasi kama sehemu ya mikakati endelevu ya kupunguza msongamano katika barabara hiyo.
Pia, utaratibu mpya wa magari kufanya mzunguko katika kata ya Chipaka kurudi Tunduma umeanza kutekelezwa, hatua iliyopokelewa vizuri na madereva.
Madereva mbalimbali wanaotumia barabara hiyo wametoa maoni yao kufuatia hatua zilizochukuliwa.
Said Hassan ambaye Dereva wa gari ya mizigo
ameeleza,
"Msongamano umepungua sana. Hii imetusaidia kuepuka usumbufu na ajali."
Dereva mwingine Beatus Komba amesema,
"Mizani ya ziada imerahisisha safari zetu na kupunguza adha tulizokuwa tunapata kwa kusubiri muda mrefu. Tunashukuru Serikali kwa uamuzi huu."
Itakumbukwa kuwa Waziri Bashungwa alielekeza kuongeza mizani mitatu katika eneo la Mpemba ili kupunguza msongamano huo.
Hadi sasa, hatua zilizochukuliwa zimeleta mabadiliko makubwa na zikionesha dhamira ya Serikali kuboresha miundombinu na huduma kwa wananchi.
Kwa ujumla, jitihada hizi zimeonesha jinsi Serikali inavyoweza kuleta suluhisho la haraka na la kudumu kwa changamoto za usafiri.
Kupungua kwa msongamano katika barabara ya TANZAM ni ushahidi wa uongozi madhubuti unaolenga kuboresha maisha ya wananchi.
Comments