FAINI MILIONI 20 UKIPEKUWA SIMU YA MWENZA WAKO
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ludewa Awataka Wanandoa Kuacha Kupekua Simu za Wenza Wao
Katika juhudi za kuimarisha amani na utulivu ndani ya familia, Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ludewa, Mkoa wa Njombe, Selestin Luhende, amewashauri wanandoa kuacha tabia ya kupekua simu za wenza wao. Akizungumza na waandishi wa habari, OCD Luhende amesisitiza kuwa kitendo hicho kimekuwa chanzo cha migogoro mingi katika ndoa, migogoro inayoweza kusababisha kuvunjika kwa ndoa na madhara mengine yanayoathiri familia na jamii kwa ujumla.
Luhende ameonya kuwa kitendo cha kupekua simu ya mwenza ni kinyume cha sheria, na endapo mwanandoa atapatikana na hatia ya kufanya hivyo, anaweza kukabiliwa na adhabu kali. Sheria inatoa adhabu ya faini ya kati ya Shilingi milioni 5 hadi Shilingi milioni 20, kifungo cha miaka mitano jela, au adhabu zote kwa pamoja.
"Kila mtu anapaswa kuheshimu faragha ya mwenza wake na kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha migogoro isiyo ya lazima katika ndoa," amesema Luhende. Ameongeza kuwa ni muhimu kwa wanandoa kujenga uaminifu na kuzungumza wazi kuhusu changamoto zao badala ya kuchunguza simu za wenza wao kwa siri.
Kauli hii imepokelewa kwa hisia tofauti, huku baadhi ya wananchi wakieleza kuwa suala la kuaminiana lina nafasi kubwa katika mahusiano ya ndoa, na tabia ya kupekua simu inaweza kuashiria ukosefu wa imani. Wengine wamepongeza hatua hii ya OCD Luhende, wakisema kuwa itasaidia kupunguza migogoro isiyo ya lazima na kurejesha amani katika ndoa nyingi.
Msimamo huu wa polisi unaleta mwanga mpya katika namna wanandoa wanavyopaswa kuhusiana, huku ikisisitizwa kuwa amani na uaminifu ni misingi muhimu ya maisha ya ndoa yenye mafanikio.
Comments