IDADI YA VIFO VYA KINA MAMA NA WATOTO WAKATI WA KUJIFUNGUA VYAPUNGUA MKOANI SONGWE

 

Songwe - Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe amefungua rasmi kikao kazi maalum kinachofanyika Tunduma, kilicholenga kujadili vifo vya akina mama na watoto wachanga vitokanavyo na matatizo ya uzazi. Katika kikao hicho, Seneda aliwapongeza watumishi wa sekta ya afya kwa kazi kubwa wanayoifanya, ambayo imeleta matokeo chanya kwa kupunguza idadi ya vifo hivyo mkoani Songwe.


“Haya ni maendeleo makubwa sana kwani hata idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa kwenda hospitali ya kanda imepungua kwa kiasi kikubwa,” alisema Katibu Tawala huyo. Alieleza kuwa jitihada za serikali na utendaji mzuri wa wahudumu wa afya umeanza kuonyesha matokeo chanya katika kupunguza vifo vya mama na mtoto mkoani humo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa kwenye kikao hicho, mwaka 2022 kulikuwa na vifo 38 vya akinamama vilivyotokana na matatizo ya uzazi, huku vifo vya watoto wachanga vikiwa 320. Hata hivyo, mwaka 2023 idadi hiyo ilishuka hadi vifo 33 vya uzazi na vifo 196 vya watoto wachanga. Hii ni sawa na uwiano wa vifo 68 vya uzazi kwa kila vizazi hai 100,000 na vifo 3 vya watoto wachanga kwa kila vizazi 1,000.


Seneda alieleza kuwa matokeo hayo ni ya kujivunia ikilinganishwa na hali ya kitaifa, ambayo ina uwiano wa vifo 104 vya uzazi kati ya vizazi hai 100,000 na vifo 24 vya watoto wachanga kwa kila vizazi 


Katibu Tawala wa Mkoa alieleza kuwa mafanikio haya yanapaswa kuendelezwa na kuongeza kuwa, “Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru watumishi wote wa sekta ya afya kwa kuendelea kupambana usiku na mchana kuwahudumia wananchi wetu, hasa akina mama wanaojifungua. Hongereni sana.”


Aidha, aliwahakikishia wahudumu wa afya kuwa serikali inatambua changamoto wanazokutana nazo katika kazi yao ya kuhudumia wananchi. “Naomba nitumie fursa hii kuwatia moyo muendelee kuitumikia nchi yetu kwa uzalendo mkubwa wakati serikali ikiendelea kuzifanyia kazi changamoto hizi,” aliongeza.


Kikao hiki kimeonesha juhudi kubwa zinazofanywa na sekta ya afya mkoani Songwe katika kupunguza vifo vya mama na mtoto. Matumaini ni kwamba, kwa jitihada hizi za pamoja na uwekezaji wa serikali, idadi ya vifo itaendelea kupungua kwa kasi zaidi na kutoa fursa kwa akinamama na watoto wachanga kupata huduma bora za afya.

Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE