AJALI YA GARI WILAYANI SONGWE YAUA WATATU, YAJERUHI 15
AJALI YA GARI SONGWE YAUA WATATU, YAJERUHI 15
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limetoa taarifa kuhusu ajali mbaya ya barabarani iliyotokea Desemba 13, 2024, majira ya saa 12:30 jioni. Ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Mitsubishi Fuso Basi lenye namba za usajili T.701 DEN, mali ya Kampuni ya Mwalumengese.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, gari hilo lilipata hitilafu baada ya kupasuka kwa tairi la nyuma, hali iliyosababisha gari hilo kuacha njia, kupinduka, na kupelekea vifo vya watu watatu na majeruhi 15.
Mahali na Chanzo cha Ajali
Ajali ilitokea katika Barabara ya Mkwajuni-Mbalizi wilayani Songwe. Dereva wa gari, Omary Ally Mdachi (45), ambaye ni mkazi wa Mkwajuni, alifariki dunia papo hapo.
Watu Waliopoteza Maisha
Jeshi la Polisi limewataja waliopoteza maisha katika ajali hiyo kuwa ni:
1. Omary Ally Mdachi (45) – Dereva wa gari, mkazi wa Mkwajuni.
2. Lugano Mwakasole Asangalwisye (25) – Mkulima, mkazi wa Saza, Wilaya ya Songwe.
3. Mwanamume mmoja ambaye bado hajafahamika, mwenye umri unaokadiriwa kuwa kati ya miaka 20 hadi 25.
Aidha Jeshi hilo limebainisha kuwa majeruhi 15 wamelazwa katika Hospitali ya Mwambani, Wilaya ya Songwe. Baadhi ya majeruhi waliotajwa ni:
Simon Henry Kajambe (21) – Mkazi wa Nzowe, Mbeya
Anna Rebson Mogde (43) – Mkazi wa Mbozi, Mbeya
Frola Musa Mbegeze (15) – Mkazi wa Mkwajuni
Abel Andrew Ramadhan (38) – Mkazi wa Mbeya Mjini
Helie Maston Ntandala (40) – Mkazi wa Mbalizi, Mbeya
Noel Harifu Patam (49) – Mkazi wa Iseche, Mbeya
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Akama Shaaban, amesema uchunguzi unaendelea kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo. Aidha, Jeshi la Polisi limewataka madereva na wamiliki wa magari kuhakikisha vyombo vyao vya moto vina hali nzuri ya kiufundi kabla ya kuanza safari, pamoja na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali kama hizi.
Comments