KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA "MAMA SAMIA" KUZINDULIWA MKOANI SONGWE KESHO
Songwe, Desemba 12, 2024 – Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe inatarajia kuzindua rasmi Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya "Mama Samia Legal Aid Campaign" (MSLAC). Uzinduzi huu umefanyika katika viwanja vya CCM Vwawa na unatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika kutoa haki na msaada wa kisheria kwa wakazi wa mkoa huu.
Akizungumza kwa Niamba ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mkuu wa Wilaya ya Ileje Farida Mgomi katika Kikao na Waandishi wa habari aliwahimiza wananchi wa Songwe kuchangamkia fursa hii adimu ya kupata msaada wa kisheria bure. "Haki za msingi za binadamu hazipaswi kupuuzwa. Kampeni hii inalenga kutoa msaada wa kisheria kwa waathiriwa wa ukatili wa kijinsia, unyanyasaji, na wale waliokosa fursa ya kutetea haki zao," alibainisha.
Kampeni ya "Mama Samia Legal Aid Campaign" inalenga kuongeza ufahamu wa sheria kama chombo muhimu cha kulinda haki za binadamu.Kutoa msaada wa kisheria kwa waathiriwa wa vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia pia kuwasaidia wananchi ambao wamekuwa wakinyimwa haki zao kuimarisha uwezo wa kudhibiti maisha yao.
Huduma hizi zitakuwa zikitolewa kwa siku tisa mfululizo kupitia mabanda maalum yatakayowekwa kwenye viwanja hivyo. Baadaye, huduma hizo zitaendelea katika halmashauri zote za Mkoa wa Songwe kwa ushirikiano wa wataalamu wa sheria na taasisi husika.
Mgomi alisisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi kupata msaada huu wa kisheria. "Ofisi yangu imejizatiti kuhakikisha kila mmoja anapata haki. Tufanye kazi pamoja kuhakikisha changamoto zote za kisheria zinatatuliwa kwa ufanisi," alisema.
Kwa mujibu wa waandaaji, kampeni hii ni sehemu ya juhudi za serikali za kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa kila mtu bila kujali hali yake ya kiuchumi au kijamii.

Comments