NAIBU WAZIRI WA MAJI AZINDUA VISIMA VILIVYOJENGWA NA MBUNGE MWENISONGOLE MILIONI 65
Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, amezindua mradi wa visima viwili vilivyojengwa kwa juhudi za Mbunge wa Jimbo la Mbozi, Mheshimiwa George Mwenisongole, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Visima hivyo vyenye thamani ya shilingi milioni 65 vimejengwa katika vijiji vya Ileya na Sambewe vilivyopo Kata ya Itumpi, na vinatarajiwa kuhudumia zaidi ya wananchi 4,068.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mbunge Mwenisongole alimshukuru Naibu Waziri kwa kukubali mwaliko wake na kuwa kiongozi wa kwanza wa ngazi hiyo kutembelea vijiji hivyo tangu uhuru. Alisema visima hivyo ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono kampeni ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.
"Niliona mateso ya wananchi wangu, hususan kina mama waliokuwa wakitegemea maji ya mvua kwa msimu mzima. Leo hii tumewapa suluhisho la kudumu kwa visima hivi, ambavyo ni historia kwao. Natoa shukrani kwa wadau wote waliosaidia kufanikisha mradi huu," alisema Mwenisongole.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Kundo aliwapongeza wananchi wa Ileya na Sambewe kwa kuwa na mbunge mwenye maono. Aliwasihi kutothubutu kumuacha Mbunge Mwenisongole katika uchaguzi ujao, kwani amedhihirisha kuwa kiongozi wa mfano kwa kutumia rasilimali zake binafsi na kushirikiana na wadau katika kuwahudumia wananchi.
"Mbunge wenu ni wa mfano. Kazi hii ni ya kuigwa. Visima hivi ni ushahidi wa dhati wa kujituma kwake na kujali ustawi wa wananchi," alisema Mhandisi Kundo.
Aidha, Naibu Waziri aliagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Songwe kuhakikisha visima hivyo vinasambaza maji kwa wananchi ili huduma hiyo iwafikie kwa urahisi zaidi.
Mradi huo umeleta matumaini mapya kwa wananchi wa Ileya na Sambewe, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya uhaba wa maji safi na salama.
Comments