BODA BODA ACHINJWA MBELE YA MKEWE SONGWE


 MAUAJI ya kutisha yametokea katika kitongoji cha Kamficheni kata ya Hasamba, Wilayani Mbozi, baada ya watu wasiojulikana kudaiwa kumuua Sadick Mwashambwa (24) dereva wa Bodaboda kwa kumchinja mbele ya mke wake akiwa na mtoto mchanga.


Tukio hilo linadaiwa kutokea Septemba 24 mwaka huu, majira ya saa 11:20 usiku baada ya watu wawili wote wanaume kufika nyumbani kwa marehemu kisha kuvunja mlango na kuingia hadi chumbani ambapo walimkuta marehemu akiwa amelala na mkewe na mtoto wao mchanga na kisha kumkamata na kumchinja mbele ya mkewe na mtoto wao mchanga.


Wakizungumza na waandishi wa habari, Mtendaji wa kata ya Hasamba, Imma Sichinga na mwenyekiti wa kitongoji cha Kamficheni Justin Ngondo walithibitisha kutokea kwa tukio hilo.


Mwenyekiti wa kitongoji Ngondo alisema siku ya tukio alipata taarifa kutoka kwa jirani wa marehemu na baada ya hapo aliwafahamisha wajumbe wa serikali ya kijiji ambao kwa pamoja walifika eneo la tukio na kujionea unyama uliofanyika.


“Mke wa marehemu ambaye kwa wakati mwingi alionekana kutokuwa sawa alitueleza kuwa wauaji wa mumewe walikuwa wanaume wawili na kwamba waliingia ndani kwa kuvunja mlango na baada ya hapo walimchinja mbele yake na kisha kutoweka bila kuchukua chochote” alisimulia Ngondo.


Alisema baada ya kukuta mwili wa marehemu ukiwa umechinjwa alichukuwa jukumu la kumpigia mtendaji wa kata ambae aliwataarifu polisi.


“Baada ya polisi kufika na kufanya uchunguzi, mwili wa marehemu licha tu ya kuchinjwa pia mwili wake ulikuwa umekatwa katwa na kuwa na majeraha mengi”.


Akizungumza huku akiwa katika hali ya majonzi makubwa shangazi wa marehemu, Lydia Mwashambwa alisema walipokea taarifa za mauaji ya shangazi yake usiku wa tukio na kufika ambapo walikuta mwili wa marehemu ukiwa umechinjwa katika hali ya kinyama.


Alisema siku moja kabla ya tukio aliongea na marehemu na kumueleza kuwa ameachana na kazi ya Bodaboda.


“Juzi alikuja nyumbani akanambia kwa sasa nimeacha kazi ya Bodaboda nimeanza kufyatua tofali mbugani…sasa sijui ni kitu gani kilitokea na kumfanyia mauaji mwanangu” alisema shangazi wa marehemu huku akibubujikwa na machozi.


Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya serikali ya Vwawa, Wilayani Mbozi, Dkt. Kenneth Lesilwa, alithibitisha kupokea mwili wa marehemu wa tukio hilo na kwamba tayari timu ya wataalamu imefanyia uchunguzi na kwamba walikuwa wakisubiri kuwakabidhi ndugu.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Alex Mukama hakuweza kupatika ili kuelezea juu ya tukio hilo iwapo kama kuna mtu yeyote aliyekamatwa.



Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE